• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Wachezaji nchini kupimwa moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Jun 19, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yazindua programu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo nchini.

Programu hiyo imezinduliwa jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ushirikiano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kuanza kutoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa miguu wanawake (Twiga Stars).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema programu hiyo ijulikanayo kwa jina la Kadiolojia ya michezo imelenga kulinda afya za mioyo ya wanamichezo nchini.

“Programu hii ni ya kipekee na ya kwanza hapa nchini, itatoa huduma kwa wanamichezo wa ngazi ya kitaifa na ngazi zingine za michezo, wanajeshi wanaofanya mazoezi kila siku pamoja na watoto wa shule wanaoanza safari yao ya michezo”, alisema Dkt. Kisenge 

Dkt. Kisenge alisema uanzishwaji wa progamu hiyo ni sehemu ya kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha michezo na kuunganisha taifa na mataifa mengine kupitia michezo.

“Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha michezo inafanyika kwa hamasa katika ngazi za kitaifa na kimataifa hata kuanzisha kampeni ya goli la mama, sisi hatuna budi kumuunga mkono kwa kuhakikisha wanamichezo wetu wana afya bora ya mioyo yao na kuzuia vifo vya ghafla vinavyoweza kusababishwa na mshtuko wa moyo wa ghafla wawapo uwanjani”,

“Takwimu zinaonyesha kuwa takribani mchezaji mmoja kati ya 50,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na tatizo hilo, wengine hushindwa hata kufika hospitalini na mara nyingi vifo hivi hutokea mbele ya mashabiki kwenye viwanja vya michezo na huacha jamii ikiwa katika huzuni na mshangao”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpiara wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia alisema kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto kubwa ya vijana hasa mashuleni na katika timu za mitaani kupoteza maisha ghafla uwanjani kutokana na matatizo ya moyo ambayo hayajawahi kugunduliwa mapema.

Kwa kutambua hilo TFF pamoja na Chama cha Makadtari wa Michezo Tanzania wameungana rasmi na JKCI katika kuanzisha na kusimamia kwa pamoja Programu ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wanamichezo wakiwemo wa ligi kuu na ligi daraja la kwanza.

Wallace alisema Progarmu hiyo itahusisha mafunzo maalum kwa madaktari wa timu na wataalamu wa afya kuhusu magonjwa ya moyo yanayohusiana na michezo na kutimiza ndogo ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa kipindi kirefu katika historia ya michezo nchini.

“Tanzania tunajiandaa kwa mashindano makubwa – CHAN 2025 na AFCON 2027, ambayo ni nafasi ya kipekee kwa taifa letu kuonesha uwezo wake katika kandanda na pia kuwekeza katika afya ya wachezaji wetu. TFF inatambua kuwa mafanikio katika michezo hayawezi kupatikana bila kuwa na wachezaji wenye afya bora hasa afya ya moyo”, alisema Wallace

Wallace alisema Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wamekuwa wakisisitiza juu ya umuhimu wa uchunguzi wa moyo kabla ya wachezaji kushiriki mashindano yoyote, hii ikiwa ni sehemu ya sera za kimataifa za ulinzi wa maisha ya wachezaji.

“Sisi kama TFF, hatuwezi kubaki nyuma, tunajiunga na vyama vyote vya mpira duniani katika utekelezaji wa sera hii na kuanzisha sera mpya kua kila mwanamichezo kabla ya kujiunga na michezo lazima achunguzwe afya ya moyo nakuendelea kuchunguzwa kwa vipindi tofauti na hii ifanyike kwa ngazi zote hadi mashuleni”, alisema Wallace