• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

JKCI kuwafanyia uchunguzi wa moyo wateja wa ATC

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, May 29, 2025
image description

Wateja wanaotumia ndege ya Air Tanzania kupata ofa ya kufanya uchunguzi wa afya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Ofa hiyo itatolewa kwa wateja wanaokata tiketi daraja la biashara (Business) kwa safari za ndani ya nchi na daraja la biashara na uchumi (Business and Economy) kwa safari za nje ya nchi.

Akizungumza mara baada ya kufanya kikao na viongozi kutoka shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL) Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imeona fursa ya kushirikiana na shirika hilo kama sehemu ya kuimarisha tiba utalii nchini.

“Ndege ya Shirika la Air Tanzania sasa inasafiri nchi mbalimbali Afrika na nje ya Afrika, tukitumia fursa hii kutoa ofa ya uchunguzi wa afya kwa wateja wake tutakuza utalii tiba nchini”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema JKCI na ATCL wapo katika mkakati wa kuidhinisha makubaliano ya ushirikiano huo ambao utalifanya Shirika hilo kuwa la kwanza kuwezesha huduma za uchunguzi wa afya kwa wateja wake nchini.

“Wateja wa Air Tanzania sasa wajiandae kupata huduma bingwa na bobezi za uchunguzi wa afya katika Taasisi yetu, tunawahaidi mkitibiwa kwetu hamtaenda hospitali nyingine”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake Meneja Masoko kutoka Shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL) Christina Tungalaza alisema ushirikiano na JKCI utasaidia kuongeza wateja wanaotumia ndege hiyo na kuongeza pato la Taifa.

Christina alisema mbali na kuongeza wateja wanaotumia ndege hiyo ushirikiano huo utasaidia kupunguza wagonjwa wanaoenda nje ya nchi kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya kwa kutumia fursa hiyo kuchunguza afya zao JKCI.

 

“Tumekuwa tukipata wateja wanaotumia ndege yetu kwenda nje ya nchi kwaajili ya kufanya uchunguzi na matibabu, tukianza ushirikiano na JKCI itawapunguzia wateja wetu adha ya kufuata huduma za afya nje ya chini na kutibiwa hapa nchini”, alisema Christina.