• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Friday, May 09, 2025
image description

Msumbiji itashirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete( JKCI) kwa kuwatuma wataalamu wake kujifunza namna ya kutoa huduma za matibabu ya moyo  kwa wagonjwa ili nchi hiyo iwe uwezo wa kutoa huduma hizo kwa wananchi.

Ushirikiano mwingine ni wa kuwapeleka wagonjwa wa moyo kutibiwa katika Taasisi hiyo na kuwatuma wataalam wao kwenda  kujifunza  namna ya kutoa huduma za matibabu ya moyo na hiyo ni sehemu ya tiba utalii.

Hayo yamesemwa leo na Mke wa Rais wan chi hiyo Mhe.  Mama Gueta Selemane Chapo alipotembelea taasisi hiyo leo  iliyopo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Mhe. Mama Gueta alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inauwezo mkubwa wa kuhudumia wagonjwa wa nje 2,000 na  kulaza wagonjwa 100 kwa wiki.

"Hospitali yetu ya Maputo haiwezi kufanya haya yote tunatamani ije ishirikiane na hospitali hii katika kutoa  huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”.

“Tunatamani hospitali kama hii iwepo katika nchi yetu na katika ukanda wa Kusini, Kati na Kaskazini ili iweze kuwahudumia mama, baba, kaka na dada zetu wenye matatizo ya moyo”.

"Tunategemea kutuma ujumbe wetu kuja kujifunza namna ya kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo, tunashukuru sana kwa kuja kwetu nchini Tanzania tumejifunza mengi”, alisema Mhe. Mama Gueta.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Mhe. Mama Gueta alikwenda kuona teknolojia ya kisasa ya matibabu ya moyo inayotumika katika taasisi hiyo ikiwemo ya kuwafuatilia wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wakiwa nyumbani kwa kuwekewa mashine ya  Dozeen chini ya  kitanda.

Dkt. Kisenge alisema kupitia mashine hiyo daktari anaona mapigio ya  moyo, presha, upumuaji na mambo mbalimbali yanayoendelea kwa  mgonjwa akiwa nyumbani na hivyo kuepusha vifo vya ghafla.

"Ameona watoto waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kwani taasisi yetu kwa mwaka inafanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa 1,000 kwa njia ya tundu dogo wagonjwa 3,000 kwa mwaka na hii ni namba kubwa na sisi ndio wa kwanza kufanya upasuaji mkubwa barani Afrika”, alisema Dkt. Kisenge.

Naye Mkurugenzi wa huduma za tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt.  Hamad Nyembea alisema lengo la ziara hiyo ya Mke wa Rais wa Msumbiji Mhe. Mama Gueta  ni kujifunza huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo na  Msumbiji itawatuma wataalamu wake  kujifunza na kuona maendeleo makubwa ambayo Tanzania imeyanfanya katika huduma za kibobezi.

"Wenzetu wa Msumbiji wamefurahi kuona tumesonga mbele katika kutoa  huduma za upasuaji wa moyo na huduma za watoto wadogo kwa ujumla wamefurahi wamejifunza wameona jinsi Serikali inavyowajali wananchi wake na kuweza kuboresha huduma za kibingwa  ili wananchi wafaidike nazo.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali ikiwezo Msumbiji ambapo kwa mwaka jana wa 2024 iliwahudumia wagonjwa 55 kutoka nchi hiyo.