• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

JKCI na NCT wasaini hati ya makubaliona kuimarisha utalii tiba nchini

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Monday, May 05, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha utalii ndani ya Tanzania unakua salama katika eneo la afya na kuchochea tiba utalili nchini.

Hati hiyo imesainiwa leo jijini Dar es Salaam katika kutafsiri maono ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwekeza katika nyanja ya afya na utalii kutengeneza mazingira ya kidoplomasia na nchi nyingine duniani.

Akizungumza mara baada ya kusaini hati hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kupitia hati hiyo JKCI na NCT watashirikiana kutoa mafunzo kwa waongoza utalii kwa kuhusisha mafunzo ya awali ya uokoaji wa maisha yatakayowasaidia waongoza watalii kuokoa maisha ya watalii pale inapotokea changamoto.

Dkt. Kisenge alisema pia watashirikiana katika kuimarisha huduma kwa mteja hususani katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambayo kwa sasa inalenga kukuza utalii tiba kwa kuwatumia vijana wanaochukua kozi za ukarimu “customer care” kujifunza kwa vitendo na nadharia katika Taasisi hiyo.

“JKCI na NCT tunaenda kufanya ushirikiano katika kufanya tafiti na kutoa maandiko yanayohusu utalii tiba nchini ambayo kwa sasa ni ajenda ya nchi, tafiti hizi zitasaidia kutengeneza mipango endelevu katika kuchochea tiba utalii nchini”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dkt. Florian Mtey alisema lengo la makubaliano kati ya JKCI na NCT ni pamoja na kuendesha program za kuwafikia watalii na jamii kuhusu msaada wa kiafya.

Dkt. Mtey aliongeza kuwa makubaliano ya ushirikiano huo ni nyenzo ya kufanikisha na kuimarisha ubora wa huduma katika taasisi hizo mbili.

“Lengo la Serikali ni kufikia watalii milioni 5 na mapato ya Dola za Marekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025, na eneo hili la watalii wanaokuja kwaajili ya matibabu ni muhimu pia katika kufikia idadi hiyo”, alisema Dkt. Mtey

 

Ushirikiano kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Chuo cha Taifa cha Utalii ni kielelezo cha dhamira ya pamoja ya kuboresha huduma na mafunzo katika sekta ya utalii na afya.