• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Wakazi wa Zanzibar watakiwa kujitokezeni kupimwa afya ya moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Saturday, Apr 05, 2025
image description

Wakazi wa Zanzibar wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa bila malipo na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Rai hiyo imetolewa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aika Nnkya wakati akizungumza na wananchi waliofika katika uwanja wa Amaani uliopo Zanzibar kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za matibabu ya kibingwa zinazotolewa uwanjani hapo.

Huduma hizo zinatolewa kwa washiriki wa kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kilichoandaliwa na Idara za Habari - Maelezo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza kuhusu huduma hiyo Dkt. Aika alisema ni muhimu wananchi wakatumia siku nne za mkutano huo kupima afya za mioyo yao ili wajue hali zao kama wanashida waanze matibabu mapema na kama hawana shida wajue jinsi gani ya kujilinda wasipate maradhi ya moyo.

“Katika upimaji huu wale tunaowakuta na matatizo ya moyo tunawapatia dawa za kutumia pia wale ambao wana matatizo makubwa tunawapa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”.

“Katika siku ya kwanza ya upimaji tumeona watu 64 kati ya hao watu watano tumewakuta na matatizo ya kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo na tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”, alisema Dkt. Aika.

Nao wakazi wa Zanzibar waliopata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo walishukuru kwa huduma hiyo na kusema kuwa imewasaidia kufahamu hali za mioyo yao.

“Nilikuwa na tatizo la presha kuna kipindi niliacha kutumia dawa baada ya presha yangu kukaa sawa, leo nimekuja kupima nimekutwa presha iko juu pia moyo wangu umeanza kutanuka. Daktari amenipa elimu ya matumizi sahihi ya dawa za presha nitaenda kuzingatia yote niliyoambiwa”, alisema Ally Amoor mkazi wa Mlandege.

“Nashukuru sana nimefika hapa nimepata huduma za matibabu na nimepewa dawa bure bila malipo yoyote yale, ninawaomba wananchi wenzangu mtumie nafasi hii kuja kupima na kujua afya zenu zikoje”, alishukuru Asha Salum mkazi wa Makunduchi.

Kikao kazi hicho cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kinakwenda sambamba za zoezi la utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali zinatolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Hospitali ya Rufaa Lumumba.