Tanzania Kushirikiana na Burkina Faso matibabu ya moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, Feb 08, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na nchi ya Burkina Faso kuwajengea ujuzi wa ubingwa bobezi wa matibabu ya moyo wataalamu wa afya wa nchi hiyo.
Hayo yamesema na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge baada ya kukutana na ujumbe wa wataalamu wa afya na washauri wa Rais wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traore jana Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge alisema Rais wa Burkina Faso baada ya kuona maendeleo makubwa yanayofanywa na taasisi hiyo akaamua kutuma ujumbe huo ili waweze kuona na wao waende kuanzisha taasisi kama hiyo.
“Taasisi hii ni moja ya taasisi kubwa barani Afrika kutoa na huduma za matibabu bobezi ya moyo tunayoyatoa, Burkina Faso wameamua kuitumia taasisi hii kuwakuza kama ambavyo Rais wao amekuwa akisema maendeleo ya Afrika yatajengwa na waafrika wenyewe”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema baada ya kuzungumza na ujumbe huo wamekubali kuleta wataalamu wao kujifunza JKCI, kuleta wagonjwa ambao walikuwa wakiwapeleka nchi za Ufaransa na Uturuki kwani maendeleo yaliyopo JKCI ni makubwa hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kuwapeleka nje ya Bara la Afrika.
“JKCI tutashirikiana na Burkina Faso kwa kuwapeleka wataalamu wetu kubadilishana nao ujuzi, kufanya tafiti kwa pamoja, kuwaongoza katika manunuzi ya vifaa tiba kupitia Bohari yetu ya Dawa (MSD) hivyo kuongeza kipato cha nchi yetu”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kutoka nchini Burkina Faso Adam SAWADOGO alisema baada ya kuona Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kuwa moja ya Taasisi zinazoongoza Barani Afrika kutoa huduma za kibingwa bobezi Rais wa Burkina Faso akawatuma kufika na kujionea ili waweze kuiga na kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini humo.
“Baada ya kufanya ziara katika Taasisi hii tumeona inakidhi viwango vya kimataifa, kama waafrika tunajivunia kufanya kazi na ninyi na mtakuwa ndio washirika wetu wakuu katika kufikia malengo yetu ya kuwa na Hospitali ya ubingwa bobezi wa magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Adam
Dkt. Adam alisema kwa niaba ya Rais wa Burkina Faso Kapteni Ibrahimu Traore na wanachini wake wanaushukuru uongozi wa Tanzania kwa kuwapokea na kukubali kuwasaidia kufikia malengo ya kuanzisha Hospitali ya moyo.
Naye Mratibu wa Utalii Matibabu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Asha Mahita alisema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri kwenye masuala ya afya iliyopelekea kupata tuzo ya The Gates Goalkeepers Award kama kielelezo cha matokeo makubwa yaliyopatikana kufuatia ripoti ya afya ya mwaka 2022.
Dkt Asha alisema kutokana na changamoto walizonazo Burkina Faso katika masuala ya matibabu ya moyo imepelekea kutengeneza fursa baina ya nchi hizo mbili kuboresha huduma za matibabu ya moyo.
“Kama nchi tumeweza kufungua milango zaidi kusaidia nchi nyingi za Afrika na sasa tumeenda mbali zaidi hadi Burkina Faso, yote hii tunataka kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa kitivo cha utalii wa matibabu kwa kutoa huduma bora zenye viwango vya kimataifa”, alisema Dkt. Asha
Dkt. Asha alisema Tanzania bado inaendelea kufungua milango ya kushirikiana na nchi nyingine katika masuala ya kidiplomasia pamoja na afya kwani wanatarajia kuona nchi nyingi zinafika Tanzania kwaajili ya kujifunza.