JKCI yapongezwa kwa kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo barani Afrika
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Jan 30, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepongezwa kwa kuwa moja ya taasisi zinazotoa huduma ya matibabu bingwa bobezi ya moyo katika bara la Afrika na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje ya bara la Afrika kufuata huduma hizo.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na washiriki wa mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika uliomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam waliotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati alipotembelea banda hilo raia wa Somalia Raclud Abdilz alisema moja ya kitu alichojifunza hapa nchini ni pamoja na uwepo wa Taasisi hiyo ya kibingwa inayotoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
“Nimefurahishwa na taarifa za taasisi hii kwani sikuwa naifahamu, sasa waafrika tunaweza kupata huduma ndani ya bara letu na karibu na nchi zetu tofauti na kuzifuata mbali na nchi zetu”, alisema Raclud.
Naye Salu Omari kutoka nchini Malawi aliipongeza Taasisi hiyo kwakuwa na ushirikiano mzuri na nchi ya Malawi kwani sasa wananchi wa Malawi wanapata huduma JKCI.
“Mmekuwa mkija nchini Malawi kutuletea huduma zenu, leo nimefika hapa Tanzania na kuona ambavyo nchi yenu imewekeza katika matibabu haya ya moyo”, alisema Salu.
Taasisi hiyo inapokea wagonjwa kutoka nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Visiwa vya Comoro, Msumbiji, Nigeria, Siera Leone, Zimbabwe, Uganda, Zambia, Congo, Ethiopia, Burundi nan chi zingine za nje ya bara la Afrika zikiwemo za Armenia, China, Ujerumani, India, Norway, Ufaransa, Uingereza na Marekani.