JKCI kufungua tawi DRC Congo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Feb 25, 2026
Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) imepanga kuvuka mipaka ya nchi na kufungua tawi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika kutoa huduma bingwa bobezi za matibabu ya moyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt Peter Kisenge wakati wa ziara ya Gavana wa jimbo la Maniema la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Mussa Kabwankubi Moise alipotembelea JKCI leo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge alisema JKCI inataka kusogeza huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi wa Congo kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda katika mataifa ya mbali kupata huduma hizo.
“Tunawaahidi watu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa tutatoa ushirikiano na kuwasaidi wasitumie gharama nyingi ambazo wanazitumia kupeleka wagonjwa nje ya Afrika kwa kuwasogozea huduma hizo karibu” alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Gavana wa jimbo la Maniema la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Mussa Kabwankubi Moise alisema baada ya kutembelea Taasisi hiyo ameridhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania na kuifanya JKCI kuwa kinara katika utoaji wa huduma bingwa bobezi za upasuaji wa moyo Afrika Mashariki na kati.
“Nimevutiwa sana na ubora wa huduma zinazotolewa na JKCI ni jambo la kujivunia kuona Taasisi ya Serikali ikitoa huduma za kiwango cha juu namna hii”, alisema Mhe. Moise
Mhe. Moise aliongeza kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itashirikiana na JKCI kwa kuwaleta wagonjwa waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi kutibiwa ili waweze kupunguza gharama zinazotumiwa na Serikali hiyo kuwasafirisha watu wake kwa ajili ya matibabu ya moyo katika nchi za mbali.
Naye Balozi wa Tanzania katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Juma Saidi Mshana aliipongeza menejimenti ya Taasisi hiyo kwa kushirikiana vema na nchi ya Congo katika kuimarisha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo mbili.