Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Wafanyabiashara Kariakoo Kunufaika na Huduma za Afya Baada ya JKCI Kufungua Kliniki Mpya

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Tuesday, Feb 24, 2026
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefungua kliniki mpya katika eneo la Soko Kuu la Kariakoo, hatua inayolenga kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo karibu na wafanyabiashara na wananchi wa eneo hilo.

Kliniki hiyo imeanza kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo bure kwa siku saba kwa wananchi wote watakaotembelea kabla ya kuendelea na utoaji wa huduma kwa utaratibu uliopangwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI, Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda alisema uamuzi wa kuanzisha kliniki hiyo umetokana na umuhimu wa kulinda afya ya wafanyabiashara katika eneo hilo ambalo hupokea maelfu ya watu kila siku.

“Tunatambua kuwa afya ni mtaji mkubwa kwa mfanyabiashara hivyo Serikali kupitia JKCI imewekeza katika miundombinu, wataalamu na vifaa tiba vya kisasa ili kuhakikisha huduma bora zinapatikana karibu na wananchi”, alisema Dkt. Mshinda.

Dkt. Mshinda aliwahimiza wafanyabiashara na wakazi wa Kariakoo kutumia kikamilifu kliniki hiyo kwa uchunguzi wa afya, matibabu pamoja na kupata elimu ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema kliniki hiyo imewekewa vifaa tiba vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja vikiwemo vinavyotumia teknolojia ya kisasa kuchunguza na kugundua magonjwa katika hatua mbalimbali.

Dkt. Kisenge alisema lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha watu wenye vipato vya aina zote wanapata huduma kwa urahisi kwani JKCI inafuata kauli mbiu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Kazi na Utu hivyo inajali utu wa watu.

“Kliniki hii pia itatoa huduma za tiba mtandao kwa wagonjwa watakaohitaji ushauri au ufuatiliaji bila kufika moja kwa moja hospitalini. Tunataka kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayepoteza muda au kupata madhara ya kiafya wakati huduma zipo karibu”, alisema Dkt. Kisenge.

Aliongeza kuwa kliniki hiyo itakuwa na dawati maalumu kwa wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali wanaofika Kariakoo kwa shughuli za biashara hivyo wasisite kupata huduma katika kliniki hiyo.

Naye Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA Ashraph Abdulkarim aliishukuru JKCI kwa kuwasogezea huduma za kibingwa wafanyabiasha wa Kariakoo na kuwataka wafanyabiashara hao kutumia fursa hiyo kupima afya zao mara kwa mara.

“Tunawaomba jumuiya ya wafanyabiashara kuwahamasisha watu wa kariakoo kutumia fursa hii kupima afya zenu na kupata elimu itakayowasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza”, alisema CPA Ashraph

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Severin Mushi alisema uwepo wa kliniki hiyo ni msaada mkubwa kwa eneo hilo ambalo hupokea zaidi ya watu laki moja kwa siku na ambalo awali halikuwa na huduma ya karibu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo.

“Kariakoo ni eneo lenye shughuli nyingi za kibiashara na linaweza kukumbwa na dharura za kiafya wakati wowote uwepo wa huduma hizi utasaidia kuokoa muda na maisha ya watu wengi”, alisema Mushi.

Aliongeza kuwa wafanyabiashara wa Kariakoo watapata huduma kwa gharama nafuu kulingana na utaratibu uliowekwa na JKCI huku akibainisha kuwa pia watashirikiana na taasisi hiyo katika kampeni za uchangiaji damu wakati wa Wiki ya Wafanyabiashara inayotarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu.

Kliniki ya JKCI Kariakoo ni tawi la saba la Taasisi hiyo ukiacha matawi yake mengine ambayo ni JKCI makao makuu, Kliniki ya Kawe, Kliniki ya Oysterbay, Kliniki ya Chato, Hospitali ya JKCI Dar Group na Hospitali ya Arusha Lutherani Medical Centre inayosimamiwa na JKCI.