Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

Watu zaidi ya 300 wafanyiwa uchunguzi wa afya na JKCI Tamasha la IST Festival

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Sunday, Feb 15, 2026
image description

Watu zaidi ya 300 wafanyiwa uchunguzi wa afya na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa tamasha la IST Festival lililofanyika jana katika viwanja vya Coco Beach vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Watu hao wamefanyiwa uchunguzi wa afya kwa kufanyiwa vipomo vya kuangalia viashiria vya magonjwa ya moyo, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO), Kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo (ECG), kipimo cha kuangalia magonjwa ya macho na kipimo cha kuangalia afya ya kinywa na meno.

Akizungumza wakati wa Tamasha hilo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema katika Tamasha hilo JKCI ilikuwa na kauli mbiu isemayo “Jua namba zako ikiwemo shinikizo la damu, sukari kwenye damu, na mapigo ya moyo” kuihamasisha jamii kuweza kujifahamu na kutambua viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.

“Kupitia kauli mbiu yetu tunataka kila kijana aliyeshiriki katika Tamasha hili anapoondoka aende na ujumbe huu kwa vijana wenzake ili kwa pamoja tuweze kuzuia magonjwa ya moyo ambayo yamekuwa tishio katika jamii zetu”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema asilimia 10 ya wagonjwa wote waliofanyiwa uchunguzi wa afya katika banda la JKCI wamekutwa na magonjwa mbalimbali yakiongozwa na magonjwa ya kinywa na meno hivyo kuwakata watu hao kufika katika Taasisi hiyo kwaajili ya matibabu zaidi.

“Watu wote waliokutwa na matatizo mbalimbali kupitia tamasha hili wafike katika Taasisi yetu tutawapa huduma bila gharama ili tuweze kutatua matatizo yao ambayo wengi wao hawakuwa wanafahamu kama wanayo”, alisema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila alisema kutokana na JKCI kutumia wataalamu wake mara kwa mara kufikisha huduma za uchunguzi wa afya kwa jamii ofisi yake itatoa kiasi cha Tshs. Milioni 200 kama sehemu ya kuwezesha uchunguzi wa afya kwa kuwafuata wananchi mahali walipo.

Mhe. Chalamila alisema JKCI imefanya kazi kubwa kupitia Tamasha hilo kwani kwa pamoja waliona wakiishia kufanya tamasha tu bila upimaji wangekuwa hawajawafikia wananchi na kuwasaidia ndio maana wakatoa huduma hizo za afya bila gharama.

Aidha Mhe. Chalamila aliitaka jamii kujitokeza kwa wingi kukata bima ya afya kwa wote itakayowasaidia kujilinda wakati wanahitaji kupata huduma za afya kwani bima hiyo itawawezesha kupata huduma katika hospitali kubwa ikiwemo JKCI. 

“Nimefika JKCI nimeona mazingira yalivyo mazuri, Serikali imewekeza sana katika Taasisi hii kwani ni mabingwa kweli kweli, mkiwa na bima za afya mtaweza kupatiwa huduma katika Taasisi hii”, alisema Mhe. Chalamila

Nao wananchi waliopata huduma katika banda la JKCI waliishukuru Taasisi hiyo kwa kuwafikia wananchi na kupata huduma na elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo kwani watu wengi hawana ufahamu wa kutosha kuhusiana na magonjwa ya moyo.

Denis Robert alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo ambalo alishatibiwa lakini kupitia tamasha hilo ameweza kukutana na wataalamu wa JKCI ambao baada ya kumfanyia uchunguzi wamemwambia anaendelea vizuri.

Fatuma Athumani alisema ametembelea banda la JKCI na kufanya uchunguzi wa macho na meno ambapo ameambiwa ana shida kidogo kwenye meno hivyo kupewa rufaa kufika katika Taasisi hiyo tawi la Dar Group kwaajili ya uchunguzi zaidi.

Naye Jumanne Kulwa alisema baada ya kuona tangazo kupitia TV aliona na siku nzuri ya kuonesha upendo ambapo JKCI imeonesha upendo kwa kuwapatia huduma za uchunguzi na matibabu ya afya wananchi ndio maana na yeye akafika ili aweze kuchunguza afya yake.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa na taratibu ya kufanya kambi mbalimbali za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika mikoa zaidi ya 23 lengo likiwa kusogeza huduma karibu na wananchi lakini pia kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.