Kamati ya upandikizaji moyo yakabidhi rasimu ya muongozo wa upandikizaji moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Feb 12, 2026
Kamati ya Upandikizaji wa Moyo imekabidhi muongozo wa maandalizi ya upandikizaji wa moyo ambao utatumika kama mwongozo wa kuanzisha huduma ya kupandikiza moyo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Muongozo huo umekabidhiwa hivi karibuni kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kuukabidhi iliyofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kupokea muongozo huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema amepokea muongozo huo kwaajili ya kuupitia na kwa pamoja wataufanyia marekebisho kabla ya kuuwasilisha Wizara ya afya kwaajili ya hatua inayofauata.
“Muongozo huu utasaidia kuimarisha huduma za upasuaji wa moyo na upandikizaji wa moyo nchini lakini pia utasaidia kupunguza gharama kubwa ambazo wanatumia wagonjwa wenye uhitaji wa kupandikizwa moyo”,
“Muongozo huu ni muhimu kwa Taasisi yetu kwani utakapokamilika na kuanza kutekelezwa utakuwa msaada mkubwa siyo tu kwa watanzania pekee bali pia kwa nchi jirani ambazo hazina huduma za upandikizaji wa moyo,” alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya upandikizaji moyo Dkt. Evarist Nyawawa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alisema muongozo huo umelenga kuimarisha huduma za upandikizaji wa moyo kwa kufuata viwango vya kimataifa.
Dkt. Nyawawa ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo alisema utekelezaji wa muongozo huo utahakikisha huduma za moyo zinatolewa kwa kuzingatia mifumo bora ya kitaalamu sambamba na kujifunza uzoefu kutoka vituo vikubwa vya afya vilivyopo India ambavyo vinatoa huduma za matibabu ya moyo kwa ufanisi mkubwa.
“Muongozo huu umeandaliwa ili kuweka msingi imara wa utekelezaji wa huduma za upandikizaji wa moyo nchini, kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa na uzoefu wa vituo vilivyofanikiwa katika huduma hizi,” alisema Dkt. Nyawawa.
Kamati ya Upandikizaji wa Moyo ilizinduliwa mapema mwaka jana na kupewa jukumu la kuchukua hatua za maandalizi na utekelezaji wa huduma ya upandikizaji wa moyo kushiriki katika juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za afya na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi.