JKCI kuisimamia ALMC, huduma za moyo na magonjwa alekezi zasogezwa Kaskazini
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Dec 17, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imesaini makubaliano ya kuisimamia Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kwa kipindi cha miaka 20, kwa lengo la kutoa huduma za matibabu ya moyo pamoja na magonjwa elekezi ya moyo na magonjwa mengine ya kibingwa kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa kati ya taasisi hiyo na ALMC.
Dkt. Kisenge, ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo, alisema ushirikiano huo unalenga kusogeza huduma za ubingwa na ubingwa bobezi wa matibabu ya moyo pamoja na magonjwa tegemezi karibu na wananchi, ili kupunguza gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
“Lengo kuu la makubaliano haya ni kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na magonjwa mengine kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, ambao kwa sasa hawatalazimika tena kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma hizi, kwani zitapatikana hapa ALMC,” alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa kuanzia Januari 1, 2026, JKCI itasimamia utoaji wa huduma zote za matibabu katika hospitali hiyo, huku ikiendelea kutumia rasilimali watu waliopo, sambamba na kupeleka wataalamu wake wa ubingwa bobezi, hususan madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo.
“Kwa upande wa huduma za moyo, tayari tumeanza kuwahamishia baadhi ya madaktari bingwa kutoka JKCI ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kiwango cha juu,” alisisitiza.
Dkt. Kisenge alisema kwa hatua hiyo, wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani hawana tena sababu ya kusafiri kwenda Dar es Salaam kufuata huduma za matibabu ya moyo, akiahidi kuwa chini ya uongozi wa JKCI, ALMC itatoa huduma za kiwango cha kimataifa, sawa na zile zinazotolewa katika Hospitali ya JKCI Upanga jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), Dkt. Goodwill Kivuyo, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia ombi la taasisi hiyo kushirikiana na JKCI, akisema mchakato wa kuomba ushirikiano huo ulianza tangu mwaka 2023.
“Tunamshukuru Rais kwa kusikiliza na kuridhia ombi letu. Ushirikiano huu na JKCI, ambayo ni hospitali kubwa ya kibingwa nchini, tunaamini utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na kwa Kanisa,” alisema Dkt. Kivuyo.
Aliongeza kuwa mkoa wa Arusha ni kitovu cha utalii kinachopokea wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali, hivyo uwepo wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali hiyo utasaidia pia kuwahudumia watalii watakaopata changamoto za kiafya wakiwa nchini.
Pamoja na JKCI kuisimamia ALMC katika utoaji wa huduma za matibabu, umiliki wa hospitali hiyo utaendelea kubaki chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK).