Watu 330 wafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Sunday, Oct 05, 2025
Jumla ya watu 330 kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani.
Matibabu hayo, yaliyoendelea kwa siku tatu, yamefanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo Tazara, wilaya ya Temeke.
Akizungumza na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo yanayohusiana na kazi, kutoka JKCI, Dkt. Elias Birago, alisema wananchi waliojitokeza walifanyiwa vipimo mbalimbali ikiwemo kipimo cha sukari kwenye damu, ECG (Electrocardiogram) kuangalia mfumo wa umeme wa moyo, ECHO (Echocardiogram) kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, kipimo cha shinikizo la damu, vipimo vya maabara, pamoja na ushauri wa lishe bora.
“Wananchi wengi waliofanyiwa uchunguzi walibainika kuwa na shinikizo la juu la damu. Sababu kuu ni mtindo wa maisha na kutozingatia mlo bora. Tumetoa rufaa kwa watu 259 kuudhuria kliniki zetu kwa vipimo zaidi. Pia, tumeona vijana wengi wamejitokeza kujichunguza, tunawaomba waendelee kulinda afya zao”, alisema Dkt. Birago.
Aidha, watu 96 waliweza kuonana na mtaalamu wa lishe kwa ajili ya ushauri, ambapo asilimia 77 walibainika kuwa na uzito uliokithiri unaoweza kuathiri utendaji wa moyo.
JKCI imesisitiza kuendeleza huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi, ili kuwapa fursa ya kupima afya zao, kwani wengi hawana tabia ya kufanya hivyo mara kwa mara.