Tanzania yapeleka madaktari bingwa Anjouan – Ushirikiano wa Afya waongeza tumaini kwa wananchi
-
Author:
JKCI Admin
-
Published At:
Friday, Oct 03, 2025
Serikali ya Tanzania imepeleka timu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kisiwani Anjouan vilivyopo Comoro kwa lengo la kuendeleza ushirikiano wa afya baina ya mataifa hayo mawili na kuhakikisha wananchi wa visiwa hivyo wanapata huduma za kibingwa bobezi.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya madaktari hao ofisini kwake jana Gavana wa Anjouan katika Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Dkt. Zaidou Youssouf, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwatuma wataalamu wake kwenda kuwasaidia wananchi wanaosumbuliwa na magonjwa yanayohitaji matibabu ya ubingwa bobezi.
Alisema kisiwa cha Anjouan kina idadi kubwa ya watu kuliko visiwa vingine vya Comoro na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya na kupata tiba stahiki.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutuletea wataalamu hawa nchini kwetu. Hii ni ishara ya ushirikiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili”, alisema Mhe. Gavana Dkt. Youssouf.
Aliongeza kuwa ingawa wananchi wengi wa Anjouan wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini, wamewapokea wataalamu wa afya wa Tanzania kwa mikono miwili na wameahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu alishukuru kwa mapokezi mazuri waliyoyapata na kusema kuwa mwaka jana wataalamu kutoka Tanzania walifanya kambi kubwa ya uchunguzi na matibabu katika kisiwa cha Ngazidja kwa kutoa huduma za matibabu ya kibingwa saba, ambapo jumla ya watu 2,770 walihudumiwa.
“Mwaka huu kambi ni kubwa zaidi. Huduma za kibingwa 17 zitatolewa katika hospitali kuu tatu zilizopo kisiwani Anjouan. Aidha, Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) imejumuishwa moja kwa moja na imekuja na dawa ambazo zitatolewa kwa wagonjwa wote. Dawa zitakazobaki zitaachwa kwenye hospitali ili ziendelee kutumika”, alisema Balozi Yakubu.
Aliongeza kuwa hadi sasa zaidi ya watu 1,000 wamejiandikisha kupokea huduma hizo ambazo pia zitahusisha elimu kwa umma kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, katika maeneo matatu maalumu yaliyotengwa kwa wananchi.
Mhe. Balozi Yakubu alisema siku ya jana timu ya wataalamu ilitembelea hospitali kubwa tatu zitakazotumika kutoa huduma ambazo ni Hombo, Pomoni na Bambao, kwaajili ya kuona vifaa vilivyopo na sehemu za kutolea huduma ya matibabu, huku wataalamu wengine wakitarajiwa kuwasili leo jioni.
Akizungumza kwa niaba ya wataalamu wenzake wa fya daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete alisema timu hiyo iko tayari kutoa huduma bora kwa wananchi wa Anjouan kwa kutumia ujuzi waliobarikiwa na Mungu, huku akiahidi kutoa huduma zenye weledi na upendo.
Wataalamu wanaoshiriki katika kambi hiyo wanatoka katika taasisi na hospitali kubwa sita za Tanzania ambazo ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Taasisi ya Saratani Ocean Road pamoja na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD).