JKCI na SACH wafanya upasuaji wa moyo kwa watoto 29 wa nchini Zambia
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Oct 02, 2025
Watoto 29 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wa nchini Zambia wamefanyiwa upasuaji wa moyo na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ya nchini Tanzania na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel.
Upasuaji huo uliomalizika hivi karibuni mjini Lusaka nchini Zambia umefanyika wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto ya siku sita katika Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa hospitali hiyo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule aliwapongeza wataalamu wa JKCI kwa kazi nzuri waliyoifaya na kuiheshimisha nchi ya Tanzania kwa kuweza kUvuka mipaka na kutoa huduma za kibingwa bobezi za matibabu ya moyo kwa watoto wa nchini Zambia.
Mhe. Balozi Mkingule alisema wakati wa harakati za uhuru katika nchi za Afrika wahasisi walipambana kuhakikisha ukombozi wa bara la Afrika unapatika, sasa Tanzania ipo kwenye harakati ya vita vya kiuchumi kuhakikisha inazisaidia nchi za Afrika kupata ujuzi hivyo kuwa na Afrika yenye afya na uwezo wa kutoa huduma bingwa bobezi kwa jamii zao.
“Nazidi kuwaomba muendelee kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia (NHH) kwa kuwapa mafunzo na msaada pale mnapoweza, ofisi ya ubalozi itafuatilia utekelezaji wa mkabata mliosaini nao ili yale yaliyoeleza katika mkataba muweze kuyafanyia kazi”, alisema Mhe. Balozi Mkingule
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema watoto 10 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na watoto 19 wamefanyiwa upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Dkt. Stella alisema wototo wote waliofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo wanaendelea vizuri na wengi wao baada ya upasuaji huo wamepona kabisa magonjwa ya moyo.
“Jana baada ya kuhitimisha kambi watoto 9 waliofanyiwa upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo kwenye paja tuliwaruhusu kurudi nyumbani baada ya hali zao kuendelea vizuri”, alisema Dkt. Stella.
Dkt. Stella alisema kupitia kambi hiyo wataalamu kutoka NHH wameweza kujifunza mambo mengi ikiwemo kufanya upasuaji mgumu wa moyo, kuhudumia wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo waliopo katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) na kuwatambua watoto wenye magonjwa ya moyo kwa wakati.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) Evance Mulendele alisema mafunzo waliyoyapata kupitia kambi hiyo yanaenda kuwaongezea ujuzi wataalamu wa Hospitali ya hiyo na kusaidia kupunguza idadi ya watoto wanaohitaji upasuaji wa moyo.
Dkt. Mulendele alisema idadi ya watoto wenye magonjwa ya moyo inazidi kuongezeka na uhitaji wa matibabu yakiwemo ya upasuaji wa moyo yameongezeka.
“Kupitia kambi hii tumeweza kujifunza mambo mengi, ninaamini wataalamu wetu katika kipindi cha miaka mitano sita ijayo watakuwa kama hawa wa JKCI walivyo, alisema Dkt. Mulendele.
Naye mama wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo Margareth Mwanza aliwashukuru wataalamu wote walioshiriki kumfanyia upasuaji wa moyo mtoto wake na kuokoa maisha yake.
Margareth alisema awali alipoteza tumaini kutokana na hali ya mwanae ilivyokuwa ikibadilia kila kukicha ila baada ya mwanae kufanyiwa upasuaji hali yake imekaa vizuri.
“Nina umri mdogo na nimekutana na changamoto kubwa za magonjwa ya moyo kwa mwanangu, madaktari waliniambia alikuwa na tundu kwenye moyo na mishipa yake ya damu ilikuwa imeziba, nawashukuru sana mmemfanyia upasuaji mwanangu na sasa huyu hapa anaendelea vizuri”, alisema Margareth