• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Wafanyakazi JKCI waaswa kufanya kazi kwa weledi

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Oct 02, 2025
image description

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kutumia vema nafasi walizonazo kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kujitoa kuendelea kuijenga Taasisi hiyo kwa maslahi ya umma.

Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa hafla fupi ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Shirikishi JKCI ambaye sasa ni Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Delilah Kimambo.

Dkt. Kisenge alisema umahiri wa Dkt. Delilah, uchapakazi uliotukuka, bidii yake ya kazi na uvumilivu akiwa JKCI ndio uliompa nafasi ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtendaji MHN.

“Sisi kama JKCI tunajivunia kwa kuendelea kutoa viongozi mahiri katika Taasisi yetu kwenda kuongoza Taasisi kubwa ndani na nje ya nchi, wafanyakazi wenzangu tusichoke kufanya kazi kwa bidii ili viongozi wengine kutoka hapa kwetu waendelee kuibuliwa katika nafasi mbalimbali”,

“Tunakupongeza sana kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji MNH, tutaendelea kushirikiana katika majukumu hata wakati huu ukiwa katika majukumu yako mapya ya kazi. Tunakuombea uendelee kuitumia vema karama yako ya uongozi hasa katika ufuatiliaji”, alisema Dkt. Kisenge.

Akitoa neno la shukrani Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Delilah Kimambo alisema ushirikiano mzuri na wafanyakazi wa taasisi hiyo ndio uliomfanya asimame vema kwenye nafasi yake na hata kuaminiwa katika nafasi kubwa zaidi.

“Ninashukuru leo nimepata nafasi ya kuwaaga na kupokea pongezi kutoka kwenu, dhamira tuliyoijenga hapa JKCI iendelee kwa dhati ili kwa pamoja tuweze kuokoa maisha ya wagonjwa wanaotutegemea”, alisema Dkt. Delilah.

Dkt. Delilah alisema JKCI ilianzishwa kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo sasa imetimiza miaka kumi ikiwa imefanya mambo makubwa ndani na nje ya nchi kutokana na umahiri wa viongozi kwa kushirikiana na wafanyakazi wengine.

Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasimali Watu JKCI Abdulrahman Muya alimpongeza Dkt. Delilah kwa bidii ya kazi aliyoionesha katika Taasisi hiyo katika kuhakikisha anasimama vyema kurugenzi ya Tiba Shirikishi.

“Ukiwa JKCI ulihakikisha Idara ya Tiba Shirikishi inafanya kazi kwa viwango vya juu kwa kufanya kazi bila kukata tamaa hata pale ulipokutana na changamoto, kwa hili tunakupongeza na kukutakia mafanikio katika majukumu yako mapya ya kazi”, alisema Muya.