• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Kambi ya matibabu ya moyo yaacha tabasamu kwa wananchi wa Shinyanga

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Saturday, Aug 30, 2025
image description

Watu 502 wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika  kambi maalum ya matibabu  iliyofanyika kwa siku tano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa  Shinyanga (SRRH).

Kambi hiyo ilifanywa na wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH).

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga (SRRH) Dkt. Luzila John alisema kati ya watu waliowaona watu wazima walikuwa 437 na watoto 65.

“Watu wote hawa walifanyiwa vipimo vya maabara vya kuangalia matatizo mbalimbali yanayoweza kusababisha magonjwa ya moyo. Watu 328 tuliwafanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na watu 287 waliwafanyia kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo”.

“Kati ya wagonjwa tuliowaona kuna ambao walikutwa na matatizo makubwa ya moyo ambayo yalihitaji matibabu ya kibingwa hivyo tumewapa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI, idadi yao ni 100 watu wazima wakiwa 63 na watoto 37”, alisema Dkt. John.

Dkt. John alisema lengo la kambi hiyo ilikuwa ni kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo karibu zaidi na wananchi wa mkoa wa Shinyanga ili kuwapunguzia gharama za usafiri za kwenda Dar es Salaam.

“Wataalamu wetu wa afya wapatao 16 wamepata mafunzo ya namna ya kufanya uchunguzi wa moyo na kutoa huduma za awali, hii ni fursa muhimu kwa hospitali ya mkoa na halmashauri za mkoa wa Shinyanga”, alisema Dkt. John.

Kwa upande wake daktari bingwa wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Mlagwa Yango alisema wagonjwa wengi waliwakuta na tatizo la Shinikizo la juu la damu, moyo kutanuna, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, matatizo ya valvu, mishipa ya damu  ya moyo na matundu kwa watoto.

Dkt. Yango alisema kufanyika kwa kambi hiyo kumewasaidia wananchi kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa haraka zaidi tofauti na ambavyo wangezifuata Dar es Salaam kwani kuna gharama za usafiri.

“Tunapowahudumia wananchi kwa kuwafuata mikoani mikoani tunawarahisishia kupata huduma na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu”, alisema Dkt. Yango.

Nao wananchi waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kuomba huduma hiyo ifanyike mara kwa mara.

“Huduma ni nzuri  ila tunaomba ziwe endelevu, mara nyingi ni gharama kubwa kwenda Dar es Salaam kupata huduma hizi hivyo ujio wa madaktari bingwa unatupunguzia mzigo mkubwa wa kufuata matibabu Dar es Salaam”, alisema Damas Kimaro mkazi wa Manispaa ya Shinyanga.

“Huduma tumepokea vizuri madaktari na wauguzi wametuhudumia bila rushwa wala usumbufu nimefurahi na ninashukuru kwa kutuletea huduma hizi, zimekuwa msaada mkubwa kwani wengi hatuna uwezo wa kusafiri hadi Dar es Salaam”, alishukuru Happiness Bwire mkazi wa Majengo Mapya.

Kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo mkoani Shinyanga ni sehemu ya programu ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services yenye lengo la kuwasogezea karibu wananchi huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.