• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Wananchi Dodoma kupimwa Moyo Maonesho ya 32 ya Nanenane

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Monday, Aug 04, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Dodoma wakati wa maonesho ya 32 ya kitaifa ya Nanenane yanayofanyika jijini humo. 

Upimaji huo unafanyika bila gharama kwa wananchi wote watakaotembelea banda la Taasisi hiyo lililopo katika maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni vilivyopo jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Johnstone Kayandabila alisema JKCI itatoa huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kuwafanyia wananchi kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG), kipimo cha kuangalia shinikizo la damu, kipimo cha kuangalia sukari kwenye damu pamoja na ushauri wa lishe kutoka kwa Afisa lishe.

Dkt. Kayandabila aliwataka wananchi wasiwe na hofu ya kufanya vipimo vya moyo kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kubadilisha mtindo wa maisha, lakini pia kuweza kukabiliana na athari za magonjwa ya moyo zinazotokea wakati wowote.

“Kinga ni bora kuliko tiba, JKCI tunaisaidia jamii kupata uelewa kuhusu magonjwa ya shinikizo la damu na magonjwa ya moyo, kufuata ushauri wa kitaalamu kuhusu lishe bora kwani magonjwa haya mara nyingi hutokana na ulaji usiofaa” alisema Dkt. Kayandabila

Kwa upande wake Dickson Mkuyu mwananchi aliyetembelea banda hilo alisema baada ya kupate elimu ya mfumo bora wa maisha ataenda kubadilisha mfumo wake wa maisha ili aweze kujikinga na magonjwa ya moyo.

“Ni vyema jamii ikatumia fursa hii kujua afya zao na kupata ushauri kutoka kwa madktari wabobezi wa magonjwa ya moyo, hii itatusaidia kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yetu “alisema Mkuyu

Naye Mary Kitoi mkazi wa Dodoma aliyefanyiwa vipimo vya moyo katika banda hilo alisema ameshauriwa kuwa anafanya uchunguzi wa afya mara kwa mara utakaomsaidia kuchukua hatua za haraka pale atakapokutwa na changamoto yoyote ya kiafya.

“Nimekuwa nikijitahidi sana kufanya mazoezi kuuweka mwili wangu kuwa na nguvu lakini nimekuwa pia nikijitahidi kula mlo unaohusisha makundi mbalimbali ya vyakula hivyo kama nitaendelea na mtindo huu wa maisha nitajilinda na maognjwa ya moyo”, alisema Mary