• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Wauguzi 11 wahitimu mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, May 29, 2025
image description

Maafisa Uuguzi 11 wamehitimu mafunzo ya muda mfupi ya miezi sita ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yaliyotolewa na  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa kuwahudumia wagonjwa mahututi ambao ni watu wazima na watoto hasa wanaohitaji uangalizi wa karibu.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo jana jijini Dar es Salaam  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kati ya wanafunzi 11 waliohitimu mwanafunzi mmoja alijifunza namna ya kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba na kupandikiza vifaa visaidizi vya moyo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.

“Leo tumeshuhudia wanafunzi 11 wakihitimu mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi na mafunzo ya Cathlab , hii ni hatua kubwa kwetu kama taasisi tumefanikisha haya kwa juhudi za pamoja na kwa kushirikiana kwa karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” alisema Dkt. Kisenge.

“Wagonjwa mnaokwenda kuwahudumia wanahitaji muda wenu, subira yenu na uelewa wenu wa kitabibu, mafanikio ya huduma hayatokani na vifaa  tiba vya kisasa peke yake , bali na namna mnavyowahudumia  wagonjwa kwa ukaribu, kwa moyo wa kujitolea na upendo ,” alikumbusha Dkt. Kisenge.

Akizungumza kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Neema Mori aliipongeza JKCI kwa uongozi thabiti na ushirikiano madhubuti katika kutoa mafunzo hayo ya muda mfupi kwa ufanisi mkubwa.

“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tunajivunia kushirikiana na JKCI katika program hizi fupi za mafunzo kwa wahudumu wa afya wa ndani na nje ya nchi” alisema Prof. Mori.

 

 

Prof. Mori alisema programu hiyo imekuwa chachu ya mabadiliko kwa washiriki wa mafunzo hayo na ni ishara ya dhamira ya taasisi hiyo katika kuboresha huduma za matibabu ya moyo ndani na nje ya nchi kwa kutumia mbinu bora za kinadharia  na za vitendo.

Kwa upande wake mtaribu wa kozi hiyo Afisa Muuguzi wa JKCI Joshua Ogutu alisema mafunzo hayo  yalianza  mwaka 2022 ambapo hadi sasa wahitimu ni 83 wameshamaliza mafunzo 10 kati yao walitoka nchini Zambia na watatu nchini Rwanda.

 Tangu wameanza  kushirikiana na UDSM hiyo ni kozi ya pili na tayari wahitimu 22 wameshamaliza mafunzo hayo ambapo wahitimu 11 walitoka Zambia na  saba kutoka Rwanda.

  “Katika kozi hii wahitimu sita wamefanya mafunzo ya kuwahudumia watoto wadogo, mmoja mafunzo ya Cathlab na wengine walijifunza jinsi ya kuwahudumia wagonjwa watu wazima”. 

“Tumeshatangaza kozi nyingine ambayo itaanza katikati ya mwezi wa saba tunatarajia kuwa na wanafuzi 24 kati ya hao 12 watatoka nchini Rwanda na wanne watatoka Zambia ninawaomba wale ambao hawajaomba waombe ili wapate mafunzo haya muhimu ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura”, alisema Ogutu. 

Naye mwanafunzi bora katika kozi hiyo Afisa Muuguzi Yusuph Kyando  kutoka hospitali ya Ikonda, Makete alisema mafunzo hayo yamemuongezea ujuzi yeye na wenzake na watatumia ujuzi huo kuwahudumia wagonjwa na kuwafundisha wenzao.

 “Tumeweza kujifunza kwa kina jinsi ya kuwahudumia wagonjwa walioko katika hali mbaya za kiafya, pamoja na usimamizi wa dharura unaohitaji huduma za karibu na uangalizi wa haraka,” alisema Kyando. 

Kyando alisema wamepata maarifa mapya na mbinu za kitaalamu za kuwahudumia wagonjwa na kuomba Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuanzisha kozi nyingine nyingi zenye uhitaji mkubwa katika sekta ya afya.

Mafunzo haya ya muda mfupi ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi ni sehemu ya mkakati wa JKCI wa kujenga uwezo wa ndani kwa wataalamu wa afya nchini na katika ukanda wa Afrika kwa kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wagonjwa zinazingatia viwango vya juu vya kitaalamu vyenye ubora wa  kimataifa.