Uwekezaji sekta ya afya wawezesha utalii tiba nchini
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Monday, May 05, 2025
Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya ikiwemo kununuliwa kwa vifaa tiba vya kisasa na kusomesha wataalamu kumewezesha kutolewa kwa huduma ya utalii tiba hapa nchini.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea taarifa ya awali ya kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana nchini Comoro.
Dkt. Shekalaghe alisema wagonjwa wengi wanatoka katika nchi zao na kwenda kutibiwa katika nchi zingine kwaajili ya kufuata utaalamu na vifaa tiba vya kisasa vilivyoko huko vitu ambavyo vinapatikana hapa nchini.
“Kazi ya upimaji iliyofanyika ni kubwa na imeiheshimisha nchi yetu, tumeweza kuokoa maisha ya wenzetu waliokuwa wanachangamoto mbalimbali za kiafya pia tumeimarisha uhusiano wa muda mrefu uliopo kati yetu na Comoro kwani Tanzania na Comoro tuna uhusiano katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya”.
“Ninamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha sekta ya afya kwani ametoa fedha nyingi ambazo zimenunua vifaa tiba vya kutosha na vya kisasa pia amewasomesha wataalamu wengi katika ngazi ya ubingwa bobezi”, alisema Dkt. Shekalaghe.
Dkt. Shekalaghe alisema katika kambi hiyo madaktari bingwa kutoka hospitali ya Taifa na maalumu walikwenda katika hospitali ya Taifa ya EL Maarouf kutoa huduma mbalimbali za matibabu na uchunguzi kwa wananchi wa Comoro.
“Ninawapongeza kwa huduma mliyoitoa nchini Comoro ninawaomba muangalie namna ambavyo mtakwenda katika nchi zingine zinazotuzunguka kama vile Zambia na Congo kufanya kambi za matibabu kama walivyofanya Comoro.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge ambaye alikuwa mratibu wa kambi hiyo alisema walikwenda nchini Comoro kuimarisha utalii tiba na kuendeleza mahusiano yaliyokuwepo baina ya nchi hizo mbili.
Dkt. Kisenge alisema katika kambi hiyo ya matibabu ya siku tano waliona watu 2779 hii ikiwa na sawa na kuona watu 550 kwa siku ambapo wataalamu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), JKCI, Hospitali ya Taifa Muhimbi (MNH), Taasisi ya Saratani Ocean Road na Hospitali ya Benjamini Mkapa walitoa huduma za kibingwa bobezi za magonjwa mbalimbali kwa wananchi.
“Tunashukuru tumeokoa maisha ya wenzetu kati ya watu tulliowaona 226 walipewa rufaa ya kuja kutibiwa katika hospitali zetu ambapo hadi sasa ni asilimia 30 wameshakuja hapa nchini kutibiwa na kwa upande wa JKCI kuna ambao tumewatibu na kuwawekea vifaa visaidizi vya moyo ikiwemo betri za moyo “Pace maker”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema katika kambi hiyo walibadilishana ujuzi wa kazi na wataalamu wa afya wa Comoro, wametangaza fursa za biashara zilizopo na wametangaza huduma ya utalii tiba inayopatikana hapa nchini kwani wananchi wengi wa Comoro wanatibiwa Ufaransa hivyo waliwaeleza fursa za matibabu zinazopatikana hapa nchini.
“Nimeona hizi hospitali zetu kubwa zikishirikiana kwa pamoja tunaweza kutoa huduma kubwa ya matibabu kwa watu wengi kwa wakati mmoja ninashukuru kwa ushirikiano tulioufanya tukiwa nchini Comoro ninaomba ushirikiano huu uwe endelevu”, alishukuru Dkt. Kisenge.
Katibu wa kamati ya Utalii Tiba Abdumalik Mollel ambaye alikuwa msimamizi wa kambi hiyo ya matibabu alisema hapa nchini kuna fursa nyingi za utalii tiba jambo la muhimu ni kuzitangaza huduma za kibingwa za matibabu zinazotolewa nje ya nchi ili watu wengi wazifahamu.
“Baada ya kufanyika kwa kambi hii wataalamu kutoka Wizara ya Afya Comoro watakuja nchini kutembelea hospitali zetu na kuona miundombinu, vifaa tiba vya kisasa vilivyopo na huduma tunazozitoa kitu ambacho kitawafanya walete wagonjwa wengi kuja kutibiwa nchini”, alisema Mollel.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya aliwapongeza wataalamu hao waliokwenda nchini Comoro kutoa huduma ya matibabu na kuiomba Wizara ya Afya kuangalia namna ambavyo watashirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha utalii tiba nchini.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi alisema utalii tiba ni fursa kubwa kwa nchi ya kuinua uchumi jambo la muhimu ni kuweka mfumo wezeshi ambao utarahisisha utoaji wa huduma hiyo katika sekta za umma na sekta binafsi.