JKCI yapata tuzo mbili huduma za matibabu ya moyo katika jamii
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, Apr 05, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepata tuzo mbili za kutumia vizuri washawishi kufikisha ujumbe kwa jamii pamoja na kutoa huduma kwa jamii ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo ijulikanayo kwa jina la tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.
Tuzo hizo zimetolewa hivi karibuni na na Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST).
Taasisi hiyo imepata tuzo hizo kutokana na kampeni inazozifanya za uchunguzi na matibabu ya moyo bila malipo kwa watu wazima na watoto huku ikitumia washawishi kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu madhara ya magonjwa ya moyo na kuitaka jamii kujitokeza kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa magonjwa hayo.
Kupitia kampeni maalumu inayowafuata wananchi mahali walipo utoa huduma za tiba mkoba zinajulikana kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services zinatolewa bure bila gharama yoyote ile. Upimaji huu pia unafanyika katika maeneo ya kazi, sehemu za ibada na katika mikutano mbalimbali ya kitaaluma.
Lengo la kampeni hiyo ni kusogeza kwa karibu huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi na kutoa mafunzo ya kuwatambua wagonjwa wa moyo kwa wataalamu wa afya ambao wanashirikiana na wataalamu wenzao wa JKCI kutoa huduma kwa wananchi.
Watu wanaogundulika kuwa na matatizo ya moyo wanafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapo hapo hii ikiwa ni pamoja na kupewa dawa za kutumia na wale wanaokutwa na matatizo yatakayohitaji matibabu ya kibingwa wanapewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.
Kwa kipindi cha mwaka jana wa 2024 huduma hizo za tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan zimetolewa katika mikoa kumi na maeneo ya kazi, ibada na mikutano ya kitaaluma nane ambapo watu 13,558 watu wazima wakiwa 11,563 na watoto 1,995 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
Kati ya hao 4,613 watu wazima wakiwa 4,405 na watoto 208 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu. Wagonjwa 1,350 watu wazima 1,192 na watoto 158 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo.
Kampeni hii ambayo imefanywa na Taasisi hiyo kwa mwaka 2024 imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.6.
Taasisi hiyo pia iliamua kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wasanii ili waihamasishe jamii kuona umuhimu wa kupima afya za mioyo yao. Wasanii walifanyiwa upimaji wa kuangalia kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu, kipimo cha kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo na kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi.
Pia walipewa elimu ya matumizi sahihi ya dawa za moyo kwani wagonjwa wengi wa shinikizo la juu la damu wakitumia dawa na kuona wamepata nafuu wanaacha kitu ambacho siyo sawa kwani matumizi ya dawa za shinikizo la juu la damu ni ya kudumu.
Aidha wataalamu wa lishe waliwapa elimu ya lishe bora iliyowapa uelewa wa kufuata mtindo bora wa maisha utakaowasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo.
Wasanii waliogundulika kuwa na matatizo ya moyo walifanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapo hapo hii ikiwa ni pamoja na kupewa dawa za kutumia na wale waliokutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.
Katika kampeni hiyo iliyofanyika kwa muda wa miezi miwili ya Novemba na Desemba 2024 ulifanyika upimaji kwa wasanii 282 ambapo hadi sasa wasanii wawili kati ya wale tuliowakuta na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa wameshapatiwa huduma hiyo na wanaendelea vizuri.
Kuwatumia wasanii katika kuhamasisha wananchi kupima magonjwa ya moyo kumesaidia wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao katika kampeni mbalimbali za upimaji zinazofanywa na JKCI, Mfano mwezi Machi 2025 JKCI imefanya upimaji mkoani Arusha na kuweza kutoa huduma kwa watu 700.