JKCI yatoa mafunzo ya awali ya kuokoa maisha kwa waongoza watalii Zanzibar
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Feb 27, 2025
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika masuala ya utafiti, kinga na matibabu ya magonjwa ya moyo huku ikidhamiria kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya na utalii nchini.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui wakati wa uzinduzi wa mkutano wa tatu wa magonjwa ya moyo (CardioTan) 2025 utakaofanyika tarehe 10 hadi 12 mwezi Aprili mjini Zanzibar ulioenda sambamba na mafunzo ya siku mbili ya awali ya kuokoa maisha kwa watu wanaoongoza watalii Zanzibar.
Mhe. Mazrui alisema JKCI imekuwa na mchango mkubwa katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mdau wa karibu kushirikiana nao katika kutoa huduma za kibingwa bobezi za magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Zanzibar.
“Wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo yaliyoshindikana kutibiwa hapa Zanzibar wamekuwa wakichukuliwa na kutibiwa katika Taasisi hii. Kwa mwaka 2024 wagonjwa 624 kutoka Zanzibar wametibiwa JKCI”, alisema Mhe. Mazrui
Mhe. Mazrui alisema sambamba na uzinduzi wa mkutano huo JKCI imefanya mafunzo ya siku mbili kwa waongoza watilii Zanzibar ya kutoa huduma ya awali ya kuokoa maisha wakiwa na lengo la kuwajengewa uwezo wakuweza kutoa msaada sahihi na wa haraka pale huduma ya kwanza na ya kuokoa maisha itakapohitajika.
“Leo tumeanza na nyie waongoza watalii, hii ni fursa adhimu mkiweza kufahamu namna ya kutoa huduma hii itasaidia kuimarisha na kukuza uchumi wa nchi kwa kuweza kuingiza idadi kubwa ya watalii nchini”, alisema Mhe. Mazrui
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema JKCI imefanya uzinduzi huo ikiwa ni ishara ya kuelekea mkutano wa tatu wa magonjwa ya moyo (CardioTan) 2025.
Dkt. Waane alisema Mkutano wa CardoTan 2024 ulikuwa na mafanikio makubwa na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu baina ya wataalamu mbalimbali wa sekta ya afya nchini na kuhusisha wataalamu wa afya kutoka nchi 40 ambao walipata elimu ya magonjwa ya moyo na kujenga mashirikiano baina ya nchi hizo.
“Mkutano wa CardioTan 2024 wataalamu wa afya walipata fursa ya kuweza kubaini viashiria vya magonjwa ya moyo, uchunguzi na matibabu yake pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo katika magonjwa haya”, alisema Dkt. Waane
Dkt. Waane alisema mafunzo ya awali ya kuokoa maisha yanaenda sambamba na uzinduzi wa mkutano huu ambayo ni muendelezo wa yale yaliyokuwa wamekubalika na kutekeleza maazimio ya mkutano wa mwaka 2024 kuwasaidia wananchi na watalii wanaotembelea visiwa vya Zanzibar.
“Tunaamini kuwa mafunzo haya yataleta tija kwenye mnyororo wa thamani ya utalii pamoja na utalii tiba kwa kusaidia kuongeza utambuzi na kutoa msaada wa haraka pale inapotokea changamoto ya afya katika jamii ama kwa watalii wetu”,
“Ujuzi na uwezo wa kuokoa maisha wakati wa dharura huongeza uelewa wa afya na usalama katika jami hivyo itasaidia sekta ya utalii kwa kuhakikisha kuwa kuna watu wanaweza kutoa msaada wa haraka pale inapohitajika na kuitangaza Zanzibar kama eneo salama kwa watalii hivyo kuongeza imani kwa wageni wetu”, alisema Dkt. Waane
Naye Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Amoor Mohamed alisema mafunzo ya awali ya kuokoa maisha yanahitajika kwa kiasi kikubwa Zanzibar kwani tafiti zinaonesha kuwa sababu inayochangia kuwa na vifo vingi vya watoto wachanga, akina mama na wagonjwa wa ajili vinatokana na upungufu wa taaluma ya kuokoa maisha.
Dkt. Mohamed alisema suala la maisha halina mbadala hivyo kuwataka wataalamu wa afya na watu wenye ujuzi na mafunzo ya kutoa huduma ya kwanza wanatumia taaluma yao kurudisha maisha ya mtu ambaye moyo wake umesita.
“Tujitoe kuhakikisha tunaokoa maisha ya binadamu wenzetu. Uokozi wa maisha si lazima ufanyike Hospitali unaweza kufanyika kokote, hivyo kila mtu ahakikishe kuwa ana uwezo wakuokoa maisha ya mwenzie pale moyo unaposimama ghafla”, alisema Dkt. Mohamed