Wataalamu wa Tehama wapimwa moyo Arusha
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Feb 12, 2025
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wameweka kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wataalamu wa Tehama.
Kambi hiyo maalumu ijulikanayo kwa jila la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba Mkoba inafanyika wakati wa mkutano wa tano wa mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii leo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete alisema mwitikio umekuwa mkubwa kwani maafisa tehama wametuma fursa hiyo kujitokeza kupima afya zao.
Dkt. Salehe alisema sambamba na kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika kambi hiyo pia wanatoa elimu ya magonjwa hayo na namna ya kukabiliana nayo.
“JKCI imeamua kuwafikia wataalamu wa Tehama kama ambavyo imekuwa ikiwafikia wataalamu wa kada nyingine nchini lengo likiwa kujenga taifa lenye afya bora”,
“Tumekuja kuwapa huduma bobezi za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia mashine zetu za kisasa zinazoweza kutambua matatizo mbalimbali ya moyo msisite kufika na kupata huduma”, alisema Dkt. Salehe
Kwa upande wake mshiriki wa mkutano huo Daud Simbeye aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kufikisha huduma hizo kwa wataalamu wa Tehama kwani watu wengi hawana tabia za kufanya uchunguzi wa afya hadi pale wanapoumwa.
Daud alisema amekuwa akifanya uchunguzi wa afya yake mara kwa mara kila anapopata fursa ya kuchunguza afya hivyo akaona ni muhimu pia kutumia fursa hii ya kupima moyo wake.
“Mimi nimekuwa muumini mzuri sana wa kuchunguza afya yangu mara kwa mara, kila ninapokuta kambi za uchunguzi wa afya sisiti kupima kwani naamini kwa kufanya hivyo ninajijua zaidi na naweza kufanya maamuzi mazuri yanayoendana na afya yangu”, alisema Daud
Naye Sophia Mgaya mshiriki wa mkutano huo aliwapongeza wataalamu wanaotoa huduma kwa kuwapa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo na kuwahamasisha kuwa na mtindo bora wa maisha ili waweze kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
“Nimefurahi sana kufika katika Kliniki hii, nimepata huduma kwa muda wa dakika ishirikini nimefanyiwa vipimo na kumuona daktari lakini pia nimepata elimu ya lishe na namna ya kujilinda na magonjwa haya”, alisema Sophia