Tanzania yapaa matibabu ya moyo kimataifa
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, Jan 25, 2025
Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yanayoongoza barani Afrika katika kutoa huduma za matibabu ya kibingwa hususani matibabu ya moyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa Kliniki ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete iliyopo Oyster plaza Haile Salassie barabara ya Ali Bin Said leo jijini Dar es Salaam.
Mhe. Muhagama alisema Serikali imeendelea kufanya jitihada za uwekezaji katika sekta ya afya lengo likiwa kukabiliana na vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Kadiri siku zinavyozidi kwenda serikali imeendelea kuwekeza kwenye vifaa tiba na vifaa vya uchunguzi lakini haijasahau kuendelea kuwekeza kwenye ubingwa na ubobezi kwa wataalamu wetu ili tuweze kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wanaotuamini”,
Mhe. Mhagama alisema Kliniki ya Oystebay si tu itahudumia wageni wanaotoka nje ya nchi lakini pia ni eneo ambalo linaweza kufikika kirahisi na watanzania wanaoishi katika maeneo haya.
“Leo nimeweza kutembelea pia kliniki ya JKCI iliyopo Kawe na kukuta wananchi wengi wanapata huduma pale ambao wameishukuru sana Serikali kwa kuwapunguzia adha ya kufuata huduma mbali”, alisema Mhe. Jenista
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt Peter Kisenge aliesema JKCI imetumia zaidi ya bilioni 2.2 kuwekeza katika kliniki ya Oysterbay na Kliniki ya Kawe.
Dkt. Kisenge alisema vifaa vilivyopo katika kliniki hizo ni vya hali ya juu, pamoja na mashine ambazo zinatumia akili bandia kwa ajili ya kugundua tatizo alilonalo mgonjwa
“Kliniki yetu inatoa huduma za matibabu kupitia huduma mtandao (Tele consultation) ambapo hata kama ukiwa nje ya Tanzania unaweza kupata huduma kutoka kwa daktari wetu yeyote”,
Moja ya vitu vikubwa ambavyo vinaweza kuitambulisha taaasisi yetu kwa upekee ni pamoja na kufanya upasuaji wa kubadilisha valvu ya moyo bila kufungua kifua (TAVI Procedure) huu ni utaalamu wa hali ya juu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inaenda kuikomboa Afrika katika masuala ya moyo kwani nchi za Zambia, Malawi, Comoro na Kongo sasa zimeanza kuitumia kwaajili ya kuzijengea uwezo.