• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

JKCI kupunguza msongamano wa wagonjwa kupitia kliniki zake

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, Jan 22, 2025
image description

Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha msongamano wa wagonjwa waliopo JKCI unafanyiwa kazi kupitia kliniki mpya za taasisi hiyo zilizofunguliwa Oystebay na Kawe.

Akizungumza wakati wa kikao cha wafanyakazi jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema menejimenti ya JKCI imefanya kazi kubwa kufungua matawi hayo kutokana na idadi ya wagonjwa wa moyo kuongeza na uhitaji wa huduma za matibabu hayo kuwa kubwa.

“Kliniki za JKCI zilizopo Oysterbay na Kawe zimelenga kupunguza msongamano wa wagonjwa hapa makao makuu lakini pia kusogeza huduma karibu na wananchi ili wasipate usumbufu kufuata huduma hizi mbali na wanapoishi”, alisema Dkt. Kisenge

Dkt. Kisenge alisema JKCI imeendelea kutambulika ndani na nje ya nchi hivyo kuzifanya nchi za Afrika kushirikiana nayo katika kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na nyingine kushirikiana na JKCI katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo.

“Taasisi yetu kwa mwaka 2024 imeweza kufanya kambi ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo nchini Comoro ambapo wagonjwa zaidi ya 2000 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo na kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo nchini Zambia”, alisema Dkt. Kisenge

Aidha Dkt. Kisenge alisema mwaka 2024 JKCI ilifanya mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo ambapo zaidi ya washiriki 500 kutoka nchi zaidi ya 12 waliweza kushiriki na kubadilishana ujuzi.

Akizungumzia mifumo ya Tehama iliyopo katika Taasisi hiyo Mkuu wa Kitengo cha Tehama Lazaro Swai alisema kitengo hicho kinaendelea kuboresha mifumo hiyo kurahisisha huduma kwa wagonjwa na kupunguza matumizi ya karatasi katika kutoa huduma.

Swai alisema mifumo ya Tehama katika sekta ya afya inasaidia kutunza taarifa za mgonjwa kwa kipindi cha muda mrefu tofauti na kama taarifa hizo zikihifadhiwa kwa njia ya faili.

“Mifumo yetu inaendelea kuboresha kila siku na kuondoa changamoto zote zinazojitokeza ili tuweze kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia”, alisema Swai

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joachim Asenga aliwataka wafanyakazi wa Taasisi hiyo kufanya kazi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu za utumishi wa umma.

Asenga alisema uongozi wa JKCI unatambua mchango mkubwa unaofanywa na wafanyakazi hivyo katika bajeti ya mwaka 2025/2026 wafanyakazi watapata ongezeko katika motisha zinazotolewa na taasisi.