Wafamasia watakiwa kufanya kazi kwa kufuata mifumo na taratibu za Taasisi
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Jan 22, 2025
Wafamasia wanaoanza mafunzo kwa vitendo (Internship) katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kutumie muda wao kujifunza na kufuata mifumo na taratibu za taasisi hiyo katika kutekeleza majukumu yao.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo Dkt. Tatizo Waane wakati akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo katika hafla fupi ya kuwaaga na kuwakaribisha wafamasia wanaopata mafunzo kwa vitendo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Waane alisema JKCI ni moja ya Taasisi za Umma inayotoa huduma bobezi na za kibingwa kwa wananchi waliopo ndani na nje ya nchi hivyo kuwataka wafamasia hao kutumia taaluma zao kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo ya kitaaluma na kuwajali wagonjwa.
“Hapa ukiwa mvivu hapatakufaa kwasababu sisi hapa kliniki zetu zipo kuanzia saa kumi na moja asubuhi hadi saa mbili usiku, hivyo wakati kliniki zinaendelea huduma za famasi pia zinatakiwa kuwa wazi”, alisema Dkt. Waane
Aidha Dkt. Waane amewapongeza wafamasia waliomaliza muda wa mafunzo kwa vitendo kwa kuwa watiifu na kutekeleza majukumu yao ya kazi bila ya kuwa na vikwazo.
“Naamini kwa miezi sita mliyokuwepo hapa mmejifunza vitu vingi ambavyo vitaenda kuwasaidia huko muendako, Sisi tumewaona na hata leo tukisikia kuna nafasi ya mfamasia tupo tayari kuwapa fursa hizo kwasababu tunawajua”, alisema Dkt. Waane
Kwa upande wake mfamasia wa JKCI Buganda Leonard amewapongeza wafamasia waliomaliza mafunzo yao kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii na kuwa na moyo wa kujifunza.
Buganda alisema kwa kipindi chote cha miezi sita wafamasia hao wamekuwa watiifu na kufuata yale waliyokuwa wakielekezwa huku wakiwa sehemu ya kuleta mabadiliko katika Taasisi.
“Mnapomaliza muda wenu hapa na kwenda kutafuta kazi muende mkiwa na taswira ya yale mliyokuwa mkiyafanya hapa JKCI na kuwa mabalozi wetu wazuri kupitia yale mliyojifunza hapa”, alisema Buganda
Akitoa shukrani zake mfamasia aliyemaliza muda wa mafunzo kwa vitendo (Internship) Edington Nkuba alisema miezi sita ya kuwa JKCI imewapa mafunzo makubwa wafamasia hao kuweza kutambua magonjwa ya moyo na dawa zinazopaswa kupewa wagonjwa hao.
Edington alisema kupitia kitengo cha kutengeneza dawa wafamasia waliokuwa kwenye mafunzo wameweza kutengeneza dawa za moyo za watoto wanaohitaji dozi ndogo kabisa.
“Ukituangalia tulivyokuja na leo tunavyoondoka ni vitu viwili tofauti, tunaondoka na ujuzi wa hali ya juu kwani ukiacha masuala ya kada yetu kama wafamasia pia tumejifunza namna ya kutunza stoo za dawa, masuala ya kutafuta wazabuni wa dawa na namna ya kununua dawa, lakini pia tumejifunza masuala ya uongozi”, alisema Edington.
Naye mfamasia anayeanza mafunzo kwa vitendo katika Taasisi hiyo Nicodemus Madyedye alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja anachotegemea kuwa katika Taasisi hiyo amejipanga kujifunza na kuwa sehemu ya kuleta faraja kwa wagonjwa.
“Sisi ni wafamasia wakwanza kupewa muda wa mafunzo kwa vitendo kwa kipindi cha mwaka mmoja katika Taasisi ya hii ya Kibingwa, tumejipanga kutekeleza majukumu yetu ya kila siku kama vile tulivyoelekezwa”,
Tutaitumikia taasisi hii vyema na kuwatumikia wananchi wanaokuja kupata huduma katika taasisi lengo letu likiwa kujenga nchi yetu katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo”, alisema Nicodemus