• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Watu wenye ulemavu 188 wapima moyo Dar

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, Jan 22, 2025
image description

Watu wenye ulemavu 188 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo, sukari na shinikizo la damu.

Matibabu hayo yamefanyika jana wakati wa hafla fupi ya chakula cha mchana na zawadi kwa watu hao iliyoandaliwa na Taasisi ya Mama ongea na mwanao katika viwanja vya Karimjee vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce alisema katika upimaji huo watu wenye ulemavu 20 wamepewa rufaa kufika katika Kliniki ya Taasisi hiyo iliyopo Kawe kwaajili ya matibabu zaidi.

“Tumewakuta baadhi ya watu wana matatizo ya shinikizo la juu la damu, lakini kutokana na vipato vyao kuwa chini wanashindwa kwenda hospitali kwaajili ya matibabu ama hata wakienda na kupewa dawa mara moja hawarudi tena”, alisema Dkt. Aloyce

Dkt. Aloyce alisema kupitia hafla hiyo watu wenye ulemavu wameweza kupata huduma za afya lakini bado kuna uhitaji wa kuwa na bima za afya kwa kila mmoja ili pale wanaopopata changamoto za afya waweze kutibiwa kirahisi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama ongea na mwanao Stevene Mengele alisema Taasisi hiyo imeweza kuwakusanya watu wenye ulemavu kukaa nao pamoja na kuwapa faraja.

Stevene alisema kundi la walemavu lilisahaulika ndio maana baada ya kuwakusanya wakaona kuna umuhimu nao waweze kupimwa magonjwa ya moyo, kucheza nao pamoja na kuwapa faraja ili wajisikie kuwa sawa na wengine.

Stevene aliwapongeza wataalamu wa afya kwa kuwa na moyo wakujitoa kwa watu hao kuhakikisha wote waliohitaji huduma ya uchunguzi wa afya wamepata kwa wakati.

“Kazi ya kutibu ni ngumu, Mungu awasimamie, tunaomba sana msituache hata hapo baadaye tukiwataka tena mtukubalie ili kwa pamoja tuweze kuwafikia watu wa kundi hili kupata huduma hizi muhimu za afya”, alisema Stevene

Wakiongea mara baada ya kupima afya watu wenye ulemavu wameishukuru serikali kwa kutoa huduma hiyo kwao kwani wengi wao hawakuwahi kufanya vipimo hivyo na hawakuwa na matarajia ya kupima moyo katika maisha yao.

Joseph Jackson mkazi wa mbagala alisema hakujua kama ana tatizo la sukari hadi baada ya kupima na kupata majibu katika hafla hiyo ndio amegundua kuwa na tatizo la sukari.

“Naishukuru sana serikali yangu kwa kutusaidia kupata huduma za afya, leo nimepima magonjwa ya moyo, sukari, na shinikizo la damu na kukutwa na tatizo la sukari. nimepewa rufaa na nina ahidi kwenda kuchunguza zaidi.

Naye Agnes Mwanuke mkazi wa Temeke ameishukuru JKCI kwa kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa walemavu kwani amekuwa akisikia maumivu makali upande wa kushoto wa moyo lakini kutokana na utafutaji wake kuwa wa shida hakufikiria kwenda hospitali kutibiwa.

“Sisi watu wenye ulemavu utafutaji wetu ni washida sana hivyo kushindwa kupata kipato cha kutupeleka hospitali kupata huduma za matibabu lakini walivyotusogezea hapa tunawashukuru sana kwani tumechunguza afya zetu”, aliema Agnes.

Agnes aliomba huduma hizo zisiishie kwa walemavu hao bali taasisi iangalie namna ya kuwafikia walemavu wengine nchini ili nao waweze kupima afya zao kwani afya ndio mtaji wa maisha.