Mchengerwa asema JKCI nguzo huduma za afya AFCON
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Jan 28, 2026
Tanzania iko tayari kutoa huduma za afya za kibingwa na kibobezi kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), hatua inayoonesha dhamira ya dhati ya nchi katika kuimarisha maandalizi ya kitabibu kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, leo jijini Arusha wakati wa ziara yake ya kutembelea ALMC ambayo hivi sasa inasimamiwa na JKCI ikiwa ni maandalizi ya kitabibu kuelekea AFCON 2027.
Mhe. Waziri Mchengerwa alisema zaidi ya kuwa tukio la michezo, AFCON 2027 pia itakuwa ni fursa adhimu ya kimkakati kwa Tanzania kujitangaza kimataifa katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, afya na uwekezaji.
“Hivi sasa tunajiandaa na michuano ya AFCON, kupitia maandalizi haya, serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa tiba na kuhakikisha uwepo wa huduma za dharura za kiwango cha juu zitakazokidhi mahitaji ya wachezaji, wageni na wananchi kwa ujumla,”alisema Mhe. Waziri Mchengerwa.
Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya taasisi hizo kupitia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ni wa kimkakati, wenye tija kwa sasa na wenye manufaa makubwa kwa mustakabali wa sekta ya afya nchini.
Akizungumza kuhusu changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza, Mhe. Waziri Mchengerwa alinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazoonesha kuwa zaidi ya vifo milioni 17.5 duniani, sawa na asilimia 32 husababishwa na magonjwa ya moyo, huku Mkoa wa Arusha ukiwa ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa magonjwa hayo.
Alitoa wito kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote huku akisisitiza kuwa ni kinga muhimu ya kifedha na nyenzo ya kuokoa maisha wakati ambapo hauna fedha za matibabu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Amos Makalla, alisema mkoa huo umejipanga kikamilifu katika maandalizi ya kitabibu kuelekea AFCON 2027, huku akibainisha kuwa JKCI iko tayari kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi pamoja na wageni watakaohudhuria michuano hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dk. Peter Kisenge, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati. Alisema taasisi hiyo tayari imewahudumia zaidi ya wagonjwa 26,000 kupitia huduma ya tiba mkoba na ina matawi saba nchini.
Dk. Kisenge aliongeza kuwa JKCI imeanza kutumia teknolojia ya akiliunde (Artificial Intelligence – AI) pamoja na mifumo ya kidijitali kufuatilia maendeleo ya wagonjwa baada ya matibabu, sambamba na kufanya upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na upasuaji wa kisasa wa matundu madogo.
“Tupo katika mpango wa kuanzisha maabara kubwa yenye vifaa vya kisasa ikiwemo MRI na CT Scan. Tayari mwekezaji kutoka China ameonesha nia ya kuwekeza katika hospitali hii,” alisema.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mtaalamu wa kupandikiza vifaa visaidizi vya moyo alisema JKCI imepokea maombi ya ushirikiano kutoka nchi za Kongo na Burkina Faso katika huduma za magonjwa ya moyo na tiba utalii, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya serikali na kuiweka Tanzania katika ramani ya huduma za afya za kibingwa barani Afrika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe alisema ushirikiano kati ya serikali, taasisi za dini na sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha maandalizi ya AFCON 2027 yanafanikiwa kwa viwango vya juu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya ALMC, Peter Maduki alisema ushirikiano kati ya JKCI na Dayosisi ya Kaskazini Kati ya KKKT ni wa kipekee na umechangia kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.