Taasisi nne za Afya zashirikiana kuboresha huduma kwa wagonjwa
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Friday, Jan 23, 2026
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zimefanya kikao cha ujirani mwema leo Ijumaa, Januari 23, 2026 jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kikao hicho kimewaleta pamoja wakuu wa taasisi hizo na baadhi ya viongozi wa menejimenti, ambapo waliangalia kwa kina masuala ya uratibu wa huduma, matumizi ya miundombinu ya pamoja na uimarishaji wa mawasiliano kati ya taasisi.
Wajumbe wameweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa, hususan wale wanaohudumiwa katika taasisi jirani.
"Kwa kuwa taasisi zetu zipo eneo moja na wagonjwa wengi wanahitaji huduma zinazohusiana, ni lazima tushirikiane kwa karibu ili kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati na kwa ufanisi," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya.
Dkt. Peter Kisenge ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI alisema kikao hicho kimewapa fursa ya kujadili changamoto kwa uwazi na kuweka mikakati bora ya kuzitatua.
"Tumekubaliana kuimarisha mawasiliano na uratibu wa huduma ili kupunguza usumbufu kwa wagonjwa na kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali zilizopo," alisema Dkt. Kisenge.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo alisema kwa kushirikiana kama taasisi jirani, wataweza kubadilishana uzoefu, kuboresha mifumo ya rufaa na kuhakikisha mgonjwa anapata huduma sahihi kwa wakati unaostahili.
Aidha Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa alisisitiza kuwa chuo hicho kinaendelea kuthamini ushirikiano na taasisi jirani, jambo linalowawezesha kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya, kufanya tafiti kwa pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za vitendo.
Vikao hivi vya ujirani mwema hufanyika mara mbili kwa mwaka ambapo kikao kijacho kitafanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).