Dkt. Peter Kisenge awataka wafanyakazi ALMC kujituma
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Wednesday, Dec 17, 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, amewataka wafanyakazi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuzingatia maadili ya kazi ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Dkt. Kisenge ametoa wito huo leo wakati akizungumza na wafanyakazi wa hospitali hiyo, ambayo kuanzia tarehe 1/1/2026 itakuwa chini ya usimamizi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Alisema JKCI imejipanga kupokea mawazo bunifu na matumizi ya teknolojia kutoka kwa wafanyakazi kama sehemu ya kuimarisha utamaduni wa kazi unaolenga kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za afya.
“Tutahakikisha ubunifu unakuwa sehemu ya utamaduni wetu wa kazi. Hatutafanya kazi kwa mazoea, bali tutaweka ubunifu katika kila tunachokifanya. Pia tutaandaa mpango wa motisha (incentive plan) ndani ya bajeti kwa wafanyakazi watakaoleta ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao na tutawazawadia,” alisema Dkt. Kisenge.
Aidha, aliwapongeza wafanyakazi wa hospitali hiyo kwa kuvumilia changamoto mbalimbali na kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa bila kukata tamaa.
“Mmekuwa mkikabiliwa na changamoto nyingi, lakini mmeendelea kusimama imara kwa kuwajali na kuwahudumia wagonjwa. Mwenyezi Mungu awabariki sana,” aliongeza Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC), Peter Maduki, alisema hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uendeshaji, hususan upande wa kifedha na upatikanaji wa wagonjwa.
“Uendeshaji wa hospitali yetu umekuwa mgumu kutokana na upungufu wa fedha pamoja na idadi ndogo ya wagonjwa wanaokuja kupata huduma ukilinganisha na miaka ya nyuma,” alisema Maduki.
Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya ALMC na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni hatua muhimu ya kuikomboa hospitali hiyo kifedha na kuongeza idadi ya wananchi watakaokwenda kupata huduma.
“Tumeamua kuingia ubia na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuhakikisha hospitali yetu inaendelea kutoa huduma sasa na baadaye, huku tukilenga kuiweka katika hali imara ya kifedha kwa ajili ya uendelevu,” alisema.
Nao wafanyakazi wa Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) waliishukuru Serikali kupitia uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuchukua hatua ya kuisimamia hospitali hiyo, wakisema hatua hiyo imeleta matumaini mapya katika utoaji wa huduma za afya.
Mmoja wa wafanyakazi wa hospitali hiyo alisema ujio wa JKCI umeongeza morali na imani ya wafanyakazi katika kuboresha huduma kwa wananchi.
“Tunaishukuru sana Serikali inayoongoza na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia JKCI kwa kutusikiliza na kutupa mwelekeo mpya. Uongozi huu umetupa moyo wa kufanya kazi kwa bidii zaidi na kwa weledi,” alisema Msimamizi wa Wauguzi wa Hospitali hiyo Afisa Muunguzi Magdalena Shangay.
Mfanyakazi mwingine alisema kuwa wamepokea maelekezo na dira mpya ya kazi inayowahamasisha kujituma na kushirikiana.
“Tunatoa ahadi ya kushirikiana na uongozi mpya, kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uaminifu ili hospitali yetu iwe mfano wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wagonjwa kwa ujumla ,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi na Wakunga Tanzania (TANNA) tawi la ALMC Afisa Muuguzi Anton Patrick.
Mkataba wa ushirikiano wa miaka 20 uliosainiwa kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK) unaashiria mwanzo wa sura mpya katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini.