Tanzania Coat of Arms
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

JKCI yaandaa mpango mkakati mpya wa miaka mitano 2026/2031

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Nov 20, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inaandaa mpango mkakati wa miaka mitano wa taasisi hiyo wa mwaka 2026/2031 unaolenga kuifanya JKCI kuwa miongoni mwa taasisi bora barani Afrika na duniani katika kutoa huduma za moyo zenye viwango vya kimataifa.

Hayo yamesemwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge wakati wa kufungua mafunzo ya kuandaa mpango mkakati huo kwa viongozi na waratibu wa kuandaa mpango mkakati mpya wa  taasisi hiyo.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo alisema mpango mkakati mpya utaendana na miongozo ya Serikali, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Miaka 25 na utajikita katika matumizi ya teknolojia za kisasa, akiliunde (AI) na ubunifu katika tiba ya moyo.

“Tunaandaa mpango wa miaka mitano utakaoiwezesha JKCI kutoa huduma za kisasa, kupanua wigo wa huduma nchini na kuongeza umahiri wetu kimataifa. Pia tunalenga kuwa taasisi inayojitegemea kifedha, kuanzisha matawi katika nchi mbili za Afrika na kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa za moyo hapa nchini”,  alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Taasisi ya Moyo Jakaye Kikwete (JKCI) CPA. Agnes Kuhenga alisema mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya awamu ya tatu ya mpango mkakati wa taasisi hiyo.

“Tunajiandaa kubuni mpango utakaoendelea kuboresha huduma za moyo ili wananchi wapate huduma bora na salama. Tumepanga pia kufungua vituo vipya vya matibabu ya moyo katika mikoa ya Geita (Chato) Arusha na Dar es Salaam, kabla ya kusambaza huduma hizo katika mikoa mingine nchini”, alisema CPA. Agnes.

Akizungumza kwa niaba ya Kampuni ya Ernest & Young (EY) ambayo imetoa  mafunzo ya kuandaa mpango mkakati huo Meneja Mwandamizi Eva Mwangoka alisema kupitia mapitio ya mpango mkakati, taasisi inapata nafasi ya kujipima na kufanya maamuzi yanayoendana na mabadiliko ya dunia.

“Mpango mkakati ni dira ya taasisi. Mapitio haya yanaiwezesha JKCI kuangalia ilipotoka, ilipo na inakoelekea, ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na kijamii”,  alisema Eva.

Washiriki wa mafunzo hayo pia walielezea manufaa yake ambapo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Neema Mwifunyi alisema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa kwa kina mpango mkakati uliopita na kuongeza ushiriki wa watumishi katika maandalizi ya mpango mkakati mpya.

“Kwa kuwa tunashiriki moja kwa moja katika kuandaa mpango mkakati huu, utekelezaji wake utakuwa rahisi na wenye tija zaidi kwa sababu kila mtumishi atauelewa vizuri”, alisema Neema .

Naye Kaimu Mkuu wa Idara ya Wauguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Daniel Mkuyu alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa wa viongozi kuhusu mwelekeo wa taasisi na yatachochea ufanisi wa kazi.

“Tunajua sasa tunakoelekea. mafunzo haya yataboresha huduma kwa wagonjwa na kuongeza uwajibikaji. Natarajia matokeo makubwa kupitia mpango mkakati huu mpya”, alisema Mkuyu.

Maandalizi ya kuandaa mpango mkakati huo yameanza rasmi kupitia mafunzo maalumu yaliyotolewa kwa viongozi na waratibu wa  kuandaa mpango mkakati wa  JKCI hatua inayolenga kufanya tathmini ya mpango mkakati uliopita wa mwaka 2022/2026 na kuweka vipaumbele vipya vinavyoendana na mahitaji ya sasa ya huduma za moyo.