Wagonjwa 9 wenye matatizo ya mishipa mikubwa ya damu kutanuka na kupasuaji wafanyiwa upasuaji JKCI
-
Author:
JKCI Admin
-
Published At:
Sunday, Oct 12, 2025
Wagonjwa tisa wenye matatizo ya mishipa mikubwa ya damu kutanuka na kupasuka wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa kurekebisha na kupandikiza mishipa ya damu iliyohitaji kubadilishwa.
Upasuaji huo ulikuwa ukifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani umefanyika katika kambi maalumu ya siku tano na kumalizika mwishoni mwa wiki.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha kambi hiyo Mkurugenzi wa Upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema mbali na kufanyika kwa upasuaji huo mkubwa, kambi hiyo pia ililenga kutoa mafunzo ya vitendo kwa wataalamu wa afya ili kuongeza ujuzi na kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka Marekani.
“Huu ni mwaka wa saba mfululizo wa ushirikiano wetu pamoja na Shirika la Cardiostart International, wataalamu hawa ni madaktari bingwa wanaotoa huduma katika kliniki maarufu za moyo nchini Marekani hivyo kwa kufanya kazi nao tunapata ujuzi mkubwa”, alisema Dkt. Angela.
Dkt. Angela alisema wataalamu hao pia walileta vifaa tiba vya kisasa vilivyotumika wakati wa upasuaji kuwasaidia wagonjwa kupata huduma bora na kupunguza gharama za matibabu.
“Kwa sasa JKCI ni kituo pekee kinachotoa huduma za upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa viwango vya juu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ambapo wagonjwa kutoka nchi jirani ikiwemo Zambia, Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Comoro na zinginezo wamekuwa wakipatiwa huduma katika Taasisi yetu”, alisema Dkt. Angela
Kwa upande wake Rais wa Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani Dkt. Miroslav Peev alisema mazingira mazuri ya kutolea huduma yaliyopo JKCI ndio yanayowafanya wataalamu kutoka shirika hilo kufika JKCI mara kwa mara kubadilisha ujuzi upande wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu pamoja na mafunzo ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na mahututi ili kwa pamoja waweze kutoa huduma bora duniani kote.
Dkt. Peev alisema wataalamu wa JKCI na wenzao kutoka hospitali nyingine walioudhuria mafunzo ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi wataenda kuimarisha huduma za afya katika hospitali zao na ndani ya nchi wote wakiwa na lengo la kusaidia kuokoa maisha.
“Wito wangu kwa watalaamu wa afya ambao wamepata mafunzo wakati wa kambi hii, muende kutumia mafunzo hayo ili kuweza kuwaokoa wagonjwa ambao wanamatatizo mbalimbali ya afya kwani wanapofika katika hospitali zenu wanakuwa na imani nanyi katika kuokoa maisha yao”, alisema Dkt. Peev
Naye daktari aliyepata mafunzo kupitia kambi hiyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Doto Sebastian aliwashukuru wataalamu kutoka Shirika la Cardiostart International kwa kuwapa ujuzi mpya katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi pamoja na mafunzo kwa wataalamu wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu.
Dkt. Doto alisema mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wa afya yanawasaidia kupata utaalamu mpya lakini pia yanawasaidia kuweza kutoa huduma itakayoendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
“Dunia ya sasa imebadilika kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kama utasoma tu darasani na kutoa huduma bila ya kupata mafunzo ya mara kwa mara utaachwa nyuma ni muhimu wataalamu wenzangu wakisikia kuna mafunzo ya kuongeza ujuzi wajitokeze ili wote tuwe katika mstari mmoja wakati wa kutoa huduma”, alisema Dkt. Doto