Watu 484 wafanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo maonesho ya madini Geita
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Oct 02, 2025
Watu 484 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya nane ya kitaifa ya madini yaliyokuwa yanafanyika katika viwanja vya maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Hayo yamesemwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu huduma walizokuwa wanazitoa kwenye maonesho hayo.
Dkt. Mayala alisema kati ya watu 484 waliofanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo 473 walikuwa watu wazima na 11 walikuwa watoto ambapo wengi wao wamekutwa na shinikizo la juu la damu, kisukari na uzito uliopitiliza.
“Wengi walikuwa hawajui kama wana haya matatizo kwahiyo kitendo cha kupima afya kimeweza kuwasaidia kupata matibabu mapema na elimu itakayowasaidia kujikinga na magonjwa hayo”, alisema Dkt. Mayala.
Dkt. Mayala alitoa wito kwa wananchi waweze kujitokeza kwa wingi pale wanaposikia taasisi hiyo ikitoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo ili kutibiwa mapema.
Nao wananchi waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika maonesho hayo walishukuru kwa huduma walizozipata na kusema kuwa zimwewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata matibabu.
“Huduma ipo vizuri ukifika unapimwa kwa dakika chache tu na huchelewi na vipimo vyao ni bure na madaktari wanatupa ushauri mzuri wa kujua afya zetu,” alisema Dayness Lucas mkazi wa Fadhili Bucha Geita.
“Nimepimwa presha na kisukari bure na nimepewa ushauri huu ni msaada mkubwa kwa kuwa vipimo hivi ni vya gharama kubwa lakini hapa tumepata bure,” alisema Neema Robin mkazi wa Geita.
“Kwa mfano huu upimaji wa moyo kikawaida ilikuwa kupata huduma yao ni mpaka uende Dar es Salaam lakini sahivi tunapata hapa karibu,” alisema Neema Robin mkazi wa Geita.
Katika maonesho hayo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilishika nafasi ya mshindi wa pili katika kundi la taasisi inayotoa huduma ya afya.