• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Watoto 28 wafanyiwa upasuaji wa moyo, Serikali yaokoa milioni 270

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Sep 18, 2025
image description

Serikali imeokoa kiasi cha shilingi milioni 270 kupitia kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka King Salman Humanitarian Aid and Relief Center nchini Saudi Arabia.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema mafanikio hayo yametokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia chini ya uongozi mahili wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kwa muda wa siku nane wamefanya upasuaji wa moyo kwa watoto waliokuwa na matatizo ya matundu kwenye moyo, kurekebisha vyumba vya moyo na mishipa ya damu ya moyo na kuokoa maisha yao.

“Watoto wote wanaendelea vizuri wataruhusiwa siku chache zijazo baada ya hali zao kuimarika, tunawashukuru wenzetu wa kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief cha nchini Saudi Arabia licha ya kutoa huduma ya upasuaji wa moyo wamekuja pia na vifaa tiba ambavyo vimetumika katika matibabu ya watoto hawa”,alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Abdallah Kashani aliishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wanaowapa na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ( JKCI) kwa watoto wenye matatizo ya moyo kama sehemu muhimu ya kutoa huduma za kibinadamu kwa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Balozi Abdallah Kilima alisema serikali inaunga mkono jitihada zinazofanywa na wataalamu wa upasuaji wa moyo kutoka nchini Saudi Arabia.

“Shukrani ziende kwa mfalme wa Saudi Arabia na madaktari ambao wamekuwa tayari kuja Tanzania kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto upasuaji ambao ni mgumu kufanyika na kuchukuwa muda mrefu lakini tumeona kuna upasuaji umechukuwa muda mfupi na tunashuhudia mafanikio makubwa”, alisema Balozi Kilima.

Naye Kiongozi wa Timu ya watalaamu kutoka Kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief cha nchini Saud Arabia Aijohara Hamza alisema mafanikio waliyoyapata ya kuwatibu watoto yametokana na ushirikiano mzuri wanaoupata kutoka kwa watalaamu wenzao wa JKCI na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali ya Tanzania katika taasisi hiyo.

“Tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kuwafanyiwa upasuaji wa moyo watoto 28 na wote wametoka salama kwani ni furaha yetu sisi kuona tunaokoa maisha ya watoto na kurudisha tabasamu kwenye familia zao”, alisema Dkt. Aijohara.

Wazazi wa watoto ambao wametibiwa katika kambi hiyo waliwashukuru wataalamu hao kwa kuokoa maisha ya watoto wao baada ya kuteseka kwa muda mrefu na ugonjwa wa moyo uliokuwa unawasumbua.

“Mtoto wangu aligundulika kuwa na matatizo ya moyo miaka miwili iliyopita na niliambiwa matibabu yake yatagharimu kiasi cha shilingi milioni tisa lakini nimelipia shilingi milioni moja fedha zingine nimepata msamaha wa matibabu na mtoto amefanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri”, alisema Mwaija Juma.

“Namshukuru Mungu mwanangu amepona peke yangu nisingeweza kabisa kumudu gharama za matibabu lakini nawashukuru madakatari, wauguzi na wataalamu wote wa afya kwa kurejesha furaha kwangu na kwa mtoto wangu”, alisema Asha Omar.