JKCI yapewa jukumu kuu: Kuinua huduma za moyo barani Afrika
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Thursday, Sep 11, 2025
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepewa wito wa kutumia utaalamu wake wa kibingwa kuendeleza hospitali mbalimbali barani Afrika zinazotoa huduma za matibabu ya moyo, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi wa bara hilo kupata huduma za matibabu nje ya Afrika na kuimarisha uwezo wa ndani wa kuhudumia wagonjwa.
Rai hiyo imetolewa jana jijini Lusaka na Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na Shirika la Save a Child’s Heart (SACH) la nchini Israel na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH).
Mhe. Luteni Generali Mkingule alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) ni wakati wao sasa kushirikiana na kugawana ujuzi walionao kwa maslahi ya nchi zao na Afrika kwa ujumla.
“Afrika tunayoitaka ni ile ya mshikamano na ushirikiano, tusishindane bali tushirikishane na kubadilishana uzoefu, ujuzi na umahiri wetu kwa ajili ya ustawi wa watu wetu na maendeleo ya Afrika kwa ujumla”, alisema Mhe. Luteni General Mkingule
Aidha Mhe. Luteni General Mkingule alisema Serikali ya nchi hizo mbili inatambua na kuthamini kwa dhati msaada wanaopata kutoka nje ya nchi hususan kutoka Shirila la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel kwani watoto hawana mipaka haijalishi wapo Afrika hivyo ni vizuri wakasaidiwa kwa pamoja na kuokoa maisha yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI na NHH wamesaini makubaliano mwaka 2023 kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa bobezi za matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya kambi maalumu za upasuaji wa moyo angalau mara mbili kwa mwaka.
“Tangu kusainiwa kwa makubaliano hayo JKCI imeshatoa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi kwa wauguzi 14 kutoka Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia, huku wanne wakiendelea na mafunzo hayo sasa”.
“Tumeshafanya kambi maalumu za upasuaji wa moyo kwa watoto nne katika hospitali hii kwa kushirikiana na SACH na wadau wengine wa kimataifa, na kwa sasa timu yetu ipo hapa kwaajili ya kambi maalumu ya tano. Takriban wananchi wa Zambia 100 wamepata huduma kupitia ushirikiano huu, ambapo kati yao asilimia 43 walifanyiwa upasuaji wa moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema kwa kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake JKCI imekuwa miongoni mwa Taasisi inayotoa huduma bingwa na bobezi za matibabu ya moyo Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara hivyo inatamani kuona Taasisi nyingine zinazotoa huduma hiyo hususani za umma zinapata mafanikio ambayo taasisi hiyo imepata.
Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) Dkt. Chabwela Shumba alisema JKCI na SACH ni Taasisi mbili za kipekee zilizoamua kuungana kwa pamoja kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo waliopo nchini Zambia.
Dkt. Shumba alisema katika kambi hiyo wataalamu hao wanafanya upasuaji wa moyo wa kisasa kwa watoto ambao wataalamu wa Hospitali hiyo wasingeweza kufanya hivyo ingepelekea watoto hao kupelekwa nje ya Zambia kwaajili ya matibabu.
“Katika kambi hii tumewafanyia uchunguzi watoto zaidi ya 30 ambapo watoto 10 watafanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na watoto 20 watafanyiwa upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo kupitia mtambo wa Cathlab, alisema Dkt. Shumba.