Upimaji wa moyo wafanyika katika maonesho ya Afya Zanzibar
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Monday, May 05, 2025
Wananchi wa Mkoa wa Singida wamepongeza huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi mwaka 2025.
Maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya maonesho Mandewa mkoani Singida ambapo taasisi hiyo inatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi bila gharama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wameelezea furaha yao kutokana na huduma walizopata kutoka kwa wataalamu wa afya waliobobea na wenye uzoefu kuhusu Magonjwa ya Moyo.
Mwahija Doe, mmoja wa wananchi wa Singida waliotembelea banda la Taasisi hiyo, alisema huduma alizopata za kuchunguza moyo wake zimemfurahisha na kuwasihi wananchi wengine kutembelea banda hilo kupata fursa ya kupima mioyo yao.
“Nimepima shinikizo la damu (BP), sukari kwenye damu, nimefanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) na nimeonana na daktari bila gharama zozote, pia nimepokelewa vizuri huduma zao ni nzuri sana”, Alisema Doe.
Kwa upande wake, Seif Mwendo ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa namna ambavyo inatoa huduma kwa wananchi wa Singida kwa weledi na kwa upendo.
“Kwa leo ukiniuliza upande wangu, Taasisi hii wamekuwa namba moja, hii ni kutokana na jinsi walivyonipokea, kuniuliza maswali kuhusu afya yangu, kunipima kwa utaratibu na kunielewesha vizuri ”, Alisema Mwendo.
Wananchi hao wameonesha kuridhika na kiwango cha huduma walizopatiwa kutoka kwa wataalamu wa afya wa JKCI ambao walikuwa na usikivu na kutoa elimu kwa kina kuhakikisha kila mwananchi anaondoka na uelewa sahihi wa hali ya afya yake na kuifanya jamii kuhamasika zaidi katika kufanya uchunguzi wa afya ya moyo.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itaendelea kutoa huduma za vipimo na ushauri wa afya katika Maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi hadi tarehe 30 Aprili mwaka huu.
Katika maonesho hayo, taasisi hiyo inatoa huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu ya moyo ikiwa ni pamoja na vipimo vya moyo, ushauri wa afya, pamoja na elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya Moyo.
Huduma hizo zimeonekana kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wengi waliopata fursa ya kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu bila gharama yoyote.