• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Waandishi wa Habari watakiwa kutumia kalamu zao kuelimisha jamii magonjwa ya moyo

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Sunday, Apr 13, 2025
image description

Waandishi wa Habari watakiwa kutumia kalamu zao kusambaza habari za kuwataka wananchi kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya hasa katika masuala ya lishe, mtindo bora wa maisha, na kuepuka tabia bwete zinazoweza kusababisha magonjwa ya moyo.

Rai hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Nassor Ahmed Mazrui wakati wa kufunga mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Sea Clif & Spa Zanzibar.

Mhe. Dkt. Nassor alisema waandishi wa habari wakitumia vizuri kalamu zao zitasaidia kupunguza magonjwa ya moyo nchini kwani magonjwa hayo ni changamoto isiyo na mipaka hivyo ni wajibu wao kushirikiana na sekta ya afya kuhakikisha nchi inapambana na tatizo hilo na kuokoa maisha.

“Magonjwa ya moyo ni janga linaloweza kudhibitiwa kupitia elimu, uelewa, na ushirikiano wa kimataifa, kwa maana hiyo mkutano huo utawawezesha wadau kubadilishana uzoefu katika kupambana na magonjwa yanayotishia maisha ya watu wengi duniani”, alisema Mhe. Dkt. Nassor

Mhe. Dkt. Nassor alisema mkutano huo wa kipekee umeweza kuwakutanisha wataalamu wa afya kutoka maeneo mbalimbali duniani kujadili kwa pamoja namna ya kukuza ushirikiano katika mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo, hivyo na waandishi wa habari wakisaidia jamii itakuwa katika nafasi nzuri ya kuyaepuka magonjwa ya moyo.

 “Bado kuna kazi kubwa yakufanya ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 kwani matokeo yanaonesha kumekuwa na changamoto ya watu kutozingatia matibabu, mfano mtu mmoja kati ya watano upande wa wagonjwa wa shinikizo la damu utumia dawa wanne wanaobaki hawatumii dawa”, alisema Mhe. Dkt. Nassor

Aidha Mhe. Dkt. Nassor ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza tafiti, kuboresha matibabu na kuihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mbali na kuboresha huduma za matibabu ya moyo mkutano huu pia umelenga katika mkakati wa kutekeleza tiba utalii nchini Tanzania kwani dunia nzima imeona na kujenga imani juu ya uwezo wa JKCI katika kutoa huduma ususani matibabu ya moyo.

Dkt. Kisenge alisema mkutano huo umeudhuriwa na  mataifa 25 ikiwemo Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Rwanda, Amerika, Chile, Korea, China, Israel, Poland, Afrika Kusini, Misri, Italy, Tunisia, Zimbambwe, Ujerumani, India na Uingereza.

Aliongeza kuwa kupitia mkutano huo wakuu wa Hospitali za moyo kutoka nchi za Afrika wameweza kukutanishwa ikiwemo hospitali za moyo za Zambia, Rwanda na Uganda.

“Wakuu wa taasisi mbalimbali za kimataifa zinazojihusisha na matibabu ya moyo nao wameshiriki nasi ikiwemo Shirika la Save a Child Hearts la nchini Israel Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani, Chama cha wataalamu wa moyo kutoka bara la Amerika, pamoja na Maabara ya Chuo Kikuu cha Philips kilichopo nchini Ujerumani”, 

“Lengo la kukutana kwa wakuu wa taasisi ni pamoja na kuangalia namna ya kuboresha na kuimarisha huduma za matibabu ya moyo kupitia njia ya ushirikiano”, alisema Dkt. Kisenge

Naye Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin Mkapa Prof. Abel Makubi aliupongeza uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutokuwa na ubinafsi katika kushirikiana na wadau wengine kubadilisha ujuzi katika masuala ya magonjwa ya moyo.

Prof. Makubi alisema taasisi nyingine za afya ni sehemu ya mafanikio ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na taasisi hizo zipo tayari kuendelea kushirikiana nao kwani wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja hasa upande wa kinga na namna ya kukabiliana na magonjwa hayo.

“Hospitali ya Benjamini Mkapa imekuwa ikifanya kazi pamoja na JKCI katika kuboresha huduma za magonjwa ya moyo, na tutaendelea kushirikiana nao”, alisema Prof. Abel Makubi

Mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wenye kauli mbiu  “kuimarisha huduma za moyo barani Afrika kupitia jitihada za pamoja” umefanyika kwa siku tatu na kumalizika jana kwa kuwakutanisha wataalamu wa magonjwa ya moyo 424 kutoka nchi 25 ambapo kati yao wataalamu 107 wametoka nje ya nchi na wataalamu 317 kutoka hospitali mbalimbali nchini.