• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Wataalamu kutoka Misri wafika JKCI kubadilishana ujuzi

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Thursday, Feb 20, 2025
image description

Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka nchini Misri watembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuangalia jinsi inavyofanya kazi na kuweka mikakati ya kushirikiana na taasisi hiyo katika kutoa huduma za kibingwa bobezi ya matibabu ya moyo.

Madaktari hao wameongozwa na rais wa Chama cha madaktari wa moyo kutoka nchini humo mara baada ya kusikia mafanikio makubwa yaliyopo JKCI katika masuala ya tiba na upasuaji wa moyo. 

Akizungumza mara baada ya kuwapokea madaktari hao Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI itashirikiana na  wataalamu hao katika kujengeana uwezo na kubadilishana ujuzi  kwani Misri imekuwa katika masuala ya matibabu hayo.

“Mbali na kushiriki na wataalamu hawa katika masuala ya matibabu pia watashiriki katika mkutano wetu wa CardioTan 2025 utakaofanyika Zanzibar mwezi Aprili ambapo hadi sasa wataalamu kutoka nchi zaidi ya 40 wamehaidi kushiriki katika mkutano huo”, alisema Dkt. Kisenge

kwa upande wake rais wa Chama cha madaktari wa moyo nchini Misri Prof. Ahmed Ashraf Eissa alisema nchi hiyo imejipanga kushirikiana na nchi za Afrika  kusambaza utaalamu wa matibabu ya moyo.

“Tumejipanga kuiwezesha Afrika kutoa huduma bingwa bobezi za matibabu ya moyo kwa wagonjwa ndio maana tumekuja Tanzania kupitia Samia Foundation kuona kinachofanyika hapa na kuweza kubadilishana ujuzi”, alisema Prof. Ahmed

Prof. Ahmed alisema wataalamu wa magonjwa ya moyo wanatakiwa wanapopata ujuzi washirikiane na wenzako ili kwa pamoja waweze kuokoa maisha ya watu wanaohitaji huduma hizo.

“Leo tupo JKCI kwa mara ya kwanza baada ya kusikia mazuri mengi inayofanya taasisi hii, tumefika na tumeona, unapoingia tu unakutana na mandhari nzuri pamoja na makaribisho mazuri ambayo yananifanya nijisikie kama nipo nchini mwangu”, alisema Prof. Ahmed

Aidha Prof. Ahmed ameushukuru uongozi wa nchi ya Tanzania, uongozi wa Wizara ya Afya na uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwakaribisha na kuwapa nafasi ya kubadilishana ujuzi kwa pamoja.