Wananchi Mbeya waishukuru Serikali kuwafikishia huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Tuesday, Feb 18, 2025
Wananchi wa mkoa wa Mbeya wameipongeza Serikali kwa kufikisha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo mkoani humo zijulikanazo kwa jina la tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.
Shukrani hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na wananchi hao waliofika leo katika viwanja vya City Park Garden kwa ajili ya kupata huduma hizo zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Moses Mwambungu kutoka Kyela alisema miaka mitatu iliyopita aliandikiwa kwenda katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kufanya vipimo vya moyo lakini kutokana na uwezo wake kiuchumi kuwa mdogo alishindwa kusafiri kwenda Dar es Salaam, baada ya kusikia huduma hizo zitakuwepo mkoani Mbeya aliona atumie nafasi hiyo kupima.
“Nimefika jana kutoa Kyela nimelala katika viwanja hivi kwaajili ya kusubiri kupata huduma, nashukuru nimefanya vipimo vyote vya moyo na nimekutwa sina shida kwani miaka ya nyuma niliwahi kupima mahali nikaambiwa nina tundu kwenye moyo”.
“Baada ya vipimo nimekutwa na shida ya presha iko juu nimeandikiwa dawa za kutumia na kuelekezwa kufanya mazoezi na kula chakula bora ili presha yangu ikae sawa”, alisema Mwambungu.
Mama Ulimbaga Mwasaga mkazi wa Mwanjela ambaye alihisi mjukuu wake anaweza kuwa na shida ya moyo kwani anakohoa sana hasa kipindi cha baridi na akaona ampeleke kwa wataalamu wa moyo ili afanyiwe vipimo.
“Baada ya kufanya vipimo wamekuta mjukuu wangu yuko sawa na hana shida yoyote ya moyo daktari amesema anatatizo la aleji amemuandikia dawa za kutumia.Ninatoa wito kwa wananchi wenzangu waje kupima afya zao kwani huduma zimewafikia mlangoni waje kupima”, alisema Mama Ulimbaga.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongella alisema wataalamu wa taasisi hiyo wako katika mkoa huo kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
“Tunatoa huduma za kibingwa kwa watoto na watu wazima huduma tunazozitoa ni tunafanya vipimo vya kuangalia sukari kwenye damu, uwiano baina ya urefu na uzito, vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo na elimu ya lishe bora”, alisema Dkt. Stella.
Dkt. Stella alisema huduma hiyo inatolewa bila malipo yoyote hivyo basi aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupima afya za mioyo yao na kupata ushauri wa kitaalamu wa matumizi sahihi ya dawa za moyo na elimu ya lishe bora.