• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

JKCI yapata tuzo mzamini mkuu mkutano wa eGA

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Tuesday, Feb 11, 2025
image description

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepewa tuzo ya mdhamini mkuu wa mkutano wa tano wa mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Tuzo hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.

Tuzo hiyo imetolewa kutokana na udhamini uliofanywa na taasisi hiyo wa kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa washiriki pamoja na kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa washiriki wote bila malipo.

Katika kutoa huduma ya upimaji taasisi hiyo imeweka mashine za kisasa za kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo ambazo zinauwezo wa kuchunguza magonjwa mbalimbali ya moyo kwa watakaofanya vipimo hivyo.

Vipimo ambavyo washiriki wa mkutano huo wanapimwa ni pamoja na kipimo cha kuangalia wingi wa sukari katika damu, kipimo cha kuangalia shinikizo la damu (BP), kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), Kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG) pamoja na vipimo vya mbalimbali vya maabara.

Taasisi hiyo imekuwa ikifanya uchungunzi wa magonjwa ya moyo kwa watu mbalimbali kupitia mikutano tofauti ya kitaalamu inayofanywa na serikali pamoja na sekta binafsi lengo likiwa kufikisha huduma hizo kwa watu wengi na kuikinga jamii na magonjwa ya moyo.