• P.O Box 65141
  • +255-788-308999

Wazibwa matundu ya moyo kwa kutumia mashine ya ECHO January 19, 2025

  • Author: JKCI Admin
  • Published At: Wednesday, Jan 22, 2025
image description

Watoto watano wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo yaani matundu wamefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo bila kufungua kifua kwa kutumia mashine ya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – Echo).  

Upasuji huo umefanyika bila kutumia mashine zenye mionzo wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Fuwai iliyopo Beijing nchini China.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kambi hiyo jana jijini Dar es Salaam daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eva Wakuganda alisema upasuaji huo umekuwa na manufaa kwao kwani wameweza kupata mafunzo ambayo yameonesha kuwa na urahisi wa kufanyika kwa upasuaji na kuzuia matumizi ya mionzi.

Dkt. Eva alisema wataalamu wa JKCI wamepata mafunzo ya hatua kwa hatua kufanya upasuaji huo unaoweza kufanyika na kuleta mafanikio kwa jamii kutokana na uwezekano wake wa kufanyika hata nje ya chumba cha upasuaji.

“Upasuaji tulioufanya hapa kupitia kambi hii ni mradi mkubwa ambao unategemewa kwenda hadi vijijini, ni upasuaji ambao unaweza kufanyika hata katika mazingira magumu na kuleta matokeo chanya”, alisema Dkt. Eva

Dkt. Eva alisema mafunzo hayo yanahitajika zaidi hasa kwa wataalamu wa upasuaji mdogo wa moyo kwa watoto ili waweze kuhama kutoka kutumia mashine za mionzi hadi upasuaji bila mionzi hivyo yaendelee kutolewa mara kwa mara kwani siku moja haitoshi.

Vaileth Mkono kutoka Shinyanga ambaye mtoto wake ana tundu kwenye moyo aliwashukuru wataalamu wa JKCI na wenzao kutoka Fuwai Beijini China kwa kumfanyia upasuaji wa moyo kwa kutumia teknolojia ya kisasa kufunga tundu lililokuwepo kwenye moyo wa mtoto wake.

Vaileth alisema anajisikia furaha kuona mwanae amefanyiwa upasuaji kwani daktari alimwambia baada ya upasuaji huo mtoto atapona kabisa na kuendelea na shughuli zingine kama ambavyo watoto wasiokuwa na magonjwa hayo wanavyofanya.

“Tatizo hili limemsumbua sana mwanangu na kumfanya kushindwa  kujichanganya na wenzake kucheza hivyo kuwa mpweke lakini pia limemsababishia asianze shule hadi leo”,

“Mwanangu alianza kuumwa tangu akiwa na umri wa miezi mitatu lakini hatukujua shida hadi pale nilipoenda Hospitali ya Bugando ndio wakaniambia ana shida ya moyo na kunipa rufaa kufika hapa JKCI kwaajili ya matibabu”, alisema Vaileth

Naye Mkurugenzi Mkuu kutoka Hospitali ya Fuwai iliyopo Beijing nchini China Prof. Xiangbin Pan alisema wameleta ujuzi wa kufanya upasuaji huo hapa nchini kuwasaidia watoto wenye magonjwa ya moyo wanaohitaji huduma hiyo kutoka   maeneo ya nje ya mjini.

“Tunasema kuwasaidia watoto wanaokaa nje ya mjini tukimaanisha kuwa upasuaji huu unaweza kufanyika hata nje ya hospitali, hivyo kuwasaidia watoto ambao hawawezi kufika hapa kwaajili ya huduma hii”, alisema Prof. Pan

 

Prof. Pan alisema wataalamu kutoka Hospitali ya Fuwai wataendelea kuwapa ujuzi wataalamu wa JKCI mara kwa mara kwa kuendesha kambi maalumu za pamoja na wakati mwingine kuwapa fursa wataalamu wa JKCI kupata mafunzo hayo nchini China.