Published 2024-11-08 05:52:50 by JKCI
JKCI yapewa kifaa kinachotumika kupima moyo (Transesophageal Echocardiography (TEE) probe) kwa watoto chenye thamani ya shilingi milioni 200 na wataalamu wa afya kutoka Shirika la Save a Childs Heart lililopo nchini Israel
Published 2024-09-24 14:37:39 by JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na Hospitali ya Medanta iliyopo nchini India kubadilishana ujuzi katika fani mbalimbali za kutoa huduma za matibabu ya moyo.Ushirikiano huo umeanza kwa mara ya kwanza jana baada ya daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Medanta kufika JKCI na kuanza kutoa huduma za upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema ujio wa daktari huyo umedhamiria kuwajengea uwezo wataalamu wa JKCI na kushirikiana kwa pamoja kubadilishana ujuzi kwa kuwafanyia upasuaji wa tundu dogo wagonjwa.“Dkt. Chandra amefika jana na kushirikiana nasi kutoa huduma za upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa wawili na leo ataendelea nasi kuwafanyia upasuaji wa tundu dogo wagonjwa wengine watatu”, alisema Dkt. WaaneDkt. Waane alisema Medanta ni moja ya Hospitali kubwa zinazotoa matibabu ya moyo kwa utaalamu mkubwa na sasa imeanza kushirikiana na JKCI katika kutoa huduma mbalimbali bingwa bobezi za moyo katika upasuaji wa moyo pamoja na kupokea wataalamu wa JKCI wanaopenda kuongeza ujuzi katika fani mbalimbali za matibabu ya moyo.Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Medanta iliyopo nchini India Preveen Chandra alisema amekuwa akifanya upasuaji wa tundu dogo kwa utaalamu wa juu hivyo akaona ni wakati sasa kukutana na wataalamu wenzake kuona namna wanavyofanya upasuaji huo na kubadilishana ujuzi.“Wagonjwa tunaowatibu India wanatoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo Afrika, wagonjwa hawa tumekuwa tukiwatibu kwa kutumia utaalamu mpya kila tunapopata ujuzi mpya kama vile upasuaji wa Tavi wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu bila ya kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI)”, alisema Dkt. ChandraDkt. Chandra alisema baada ya kufanya upasuaji na wataalamu wa JKCI ameona ni Taasisi inayokuwa kwa kasi kutokana na uwekezaji wa vifaa tiba vya kisasa vinavyotumika kutoa huduma za upasuaji wa moyo.“Naamini baada ya miaka 10 ijayo taasisi hii itakuwa inafanya aina zote za upasuaji wa moyo zinazofanyika duniani, ushirikiano wetu na taasisi hii utaendelea kuhakikisha kila hatua inayopigwa duniani katika kutoa huduma hizi na hapa hatua hiyo inafanyika”, alisema Dkt. Chandra
Published 2024-09-17 07:41:09 by JKCI
Kuanza kutumika kwa bima ya afya kwa wote kutasaidia kupunguza gharama za matibabu ya kibingwa yakiwemo ya moyo na hivyo kuwaondolea wananchi mzigo mkubwa wa kulipia gharama hizo.Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipofanya ziara ya kuangalia utoaji wa huduma na mwelekeo wa taasisi hiyo tangu alipoteuliwa kuwa waziri wa afya mwezi Agosti mwaka huu. Waziri Mhagama alisema gharama za matibabu ya kibingwa ni kubwa na Serikali imekuwa na jukumu kubwa la kulipia gharama za matibabu kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kulipia lakini kuanza kutumia kwa bima ya afya kwa wote kutawasaidia wananchi kupata huduma mahali popote walipo hata kama hawatakuwa na fedha mfukoni kipindi ambacho wataugua. “Ninawaomba bima ya afya kwa wote ikianza kutumika mjiunge kwani itawasaidia kupata matibabu mahali popote pale mlipo na itasaidia kufuatilia matibabu ya mgonjwa kutoka hospitali yoyote nchini kwani mfumo wa matibabu utakaotumika utakuwa ni mmoja”. “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kusaidia mfuko unaohudumia watanzania kuweza kufikiwa na matibabu haya ya kibobezi kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 6 ili ziweze kusaidia katika utoaji wa huduma hizo na kuanzisha mfumo wa bima ya afya kwa wote”, alisema Mhe. Jenista. Aidha Waziri Mhagama aliwapongeza wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwa kazi nzuri wanazozifanya na ubunifu walionao katika kutoa tiba hapa nchini na kuona ni muhimu kuwe na mfumo wa kuzizawadia hospitali zinafanya ubunifu wa namna yoyote kila mwaka ili kuweza kuhamasisha maendeleo katika sekta ya afya nchini. Mhe. Waziri huyo wa Afya alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni taasisi pekee inayoongoza na yenye sifa na heshima ya kutoa matibabu ya kibobezi ya moyo hasa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati hivyo basi aliwaomba wataalamu wa Taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma hizo kwa kujitoa kwani wagonjwa wanawategemea wao katika kuokoa maisha yao.“Ninawasihi uongozi wa JKCI mjitahidi kukuza shughuli na huduma zinazofanywa hapa ikiwemo kutoa huduma mpya za kibingwa mara kwa mara kwa kufanya hivyo mtapata wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi na kuendelea kuimarisha utalii wa tiba kwani wagonjwa wengi watakuja kutibiwa hapa”, alisisitiza Mhe. Mhagama. Kwa upande wa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo walishukuru kwa huduma ya matibabu ya moyo wanayoipata na kusema kuwa kwa kiwango kikubwa imesaidia kuokoa maisha yao na ya watoto wao wenye matatizo ya moyo. Happy Nkinda kutoka mkoani Geita alimwambia waziri huyo wa Afya kuwa mtoto wake alikuwa akisumbuliwa na tatizo la tundu dogo kwenye moyo kwa muda mrefu na kumpeleka hospitali mbalimbali bila mafaniko mpaka pale alipopewa rufaa ya kwenda JKCI.“Namshukuru sana Mungu, mara baada ya mtoto wangu kupatiwa matibabu kwa sasa anaendelea vizuri, pia nawashukuru waatalamu wa JKCI kwa huduma zao nzuri na ushirikiano wao kipindi chote cha matibabu”, alisema Happy. “ Mtoto wangu aligunduliwa kuwa na shida ya moyo katika moja ya hospitali iliyopo mkoani Mara na kupewa rufaa kuja JKCI ambapo aligundulika kuwa na tundu kwenye moyo, namshukuru Mungu na wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa kumfanyia upasuaji na sasa anaendelea vizuri”, alisema Edna. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alimshukuru Mhe. Waziri wa Afya Jenista Mhagama kwa kutembembelea Taasisi hiyo na kuona uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo pamoja na kuwekeza katika rasilimali watu. “Taasisi yetu ni moja ya taasisi bora za afya katika nchi za Afrika Mashariki na Kati hivyo mheshimiwa Waziri amekuja kuona huduma tunazozitoa, na wagonjwa wengi aliowauliza maswali walimjibu kuwa wameridhika na huduma tunazozitoa na hii inaonesha ni jinsi gani wataalamu wa JKCI wanavyotoa huduma bora kwa wagonjwa wanaowahudumia”, alisema Dkt. Kisenge. Dkt. Kisenge alisema wao kama taasisi wataendelea kuimarisha teknolojia ya matibabu ili waweze kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa maeneo ambayo ni vigumu kwa wananchi kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu alisema kutokana na uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba na rasiimali watu uliofanyika katika taasisi hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kuleta wagonjwa kutoka nchi mbalimbali kuja kupata matibabu hapa nchini.
Published 2024-09-03 06:13:29 by JKCI
Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma nchini wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za ushauri, upimaji na matibabu ya moyo kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).Huduma hiyo ya uchunguzi iliyofanyika hivi karibuni ilitolewa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya AICC ambapo huduma zilizotolewa ni kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu, vipimo vya maabara, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa moyo.Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi viongozi hao walisema wengi wao hawana muda wa kupima afya zao hii ni kutokana na majukumu ya kazi waliyokuwa nayo lakini kutolewa kwa huduma hiyo katika kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kumewasaidia kupata muda wa kupima afya zao.“Kutokana na majukumu ya kazi kuwa mengi sisi viongozi huwa tunakosa muda wa kupima afya zetu na wengi wetu tunatumia dawa pale tunapojisikia vibaya, lakini katika kikao kazi hiki tumeletewa huduma hii muhimu ya kupima afya zetu, nimeona nami nije kupima afya yangu ili nijue nikoje”.“Ninaishauri JKCI iwe na programu ya kupima afya za moyo za wafanyakazi maofisini hata kama kuna gharama za upimaji wazijulishe taasisi husika ili zigharamie, kwa kufanya hivyo wafanyakazi wengi watafikiwa na huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo”, alisema Stanley Mwonzya Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Tumbaku Tanzania.“Tulipofika hapa tulitangaziwa kuna huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo mwenye nafasi anaweza kwenda kupima, nilifurahi kupata nafasi hii kwani kupata huduma ya upimaji wa moyo siyo jambo rahisi. Nimeonana na wataalamu na kupima vipimo vya moyo na figo namshukuru Mungu majibu yako vizuri, shida niliyonayo ni uzito mkubwa nimepewa ushauri wa kuzingatia lishe bora na kufanya mazoezi nitaenda kutekeleza ushauri niliopewa na daktari”, alishukuru Edna Mwaigomole Mwenyekiti wa Bodi ya Mamkala ya Maji Mbeya.Allen Marwa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Kahama alishukuru kwa huduma aliyoipata ya ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo amepewa elimu nzuri ya lishe ambayo imemsaidia kujua aina gani ya vyakula ale ikiwemo mbogamboga na matunda pamoja na kufanya mazoezi.“Ninawashauri wenzangu mahali popote pale watakapokuwa wanapopata nafasi ya kupima afya zao wapime na kama watakutwa na matatizo watapata matibabu mapema zaidi kuliko kusubiri tatizo limekuwa kubwa”, alisema Marwa.Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dickson Minja alisema kwa kushirikiana na hospitali ya AICC wametoa huduma za kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa viongozi na wenye shida wamewapa rufaa ya kwenda JKCI kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.“Mwitikio umekuwa ni mkubwa viongozi wengi wamekuja kupima afya zao na baadhi tumewapa rufaa kwaajili ya uchunguzi zaidi, ninatoa wito kwa washiriki wa mikutano mbalimbali pale kutakapokuwa na nafasi ya kupima afya wajitokeze kwa wingi na kupima afya”, alisema Dkt. Minja.Naye Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya AICC Arusha Dkt. Ezekiel Moirana alisema katika mikutano mbalimbali itakayofanyika jijini Arusha wataendelea kushirikiana na JKCI kutoa huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu ya magonjwa ya moyo kwani katika ukumbi wa AICC wanapokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi wanaohitaji huduma hiyo.“Zoezi hili litakuwa endelevu kwani licha ya washiriki wa mkutano kupata huduma ya upimaji wa moyo ambayo tunaitoa bila malipo yoyote yale lakini pia wataalamu wetu wanajengewa uwezo na wenzao wa JKCI wa jinsi ya kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo kwani upimaji huu tunaufanya kwa pamoja”, alisema Dkt. Moirana.
Published 2024-08-29 06:33:58 by JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) imepokea tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024.Tuzo hiyo imetolewa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa Taasisi za umma kilichoandaliwa na ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa Arusha (AICC).Tuzo hiyo imeielezea JKCI kwenda hatua moja zaidi mbele katika kufanikisha malengo ya taasisi na kusaidia taasisi zingine nazo ziweze kufikia hatua ambayo taasisi hiyo imefikia katika utoaji wa matibabu ya moyo.Akielezea tuzo hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Thobias Makoba alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita JKCI ilitoa huduma za upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua kwa wagonjwa 654 ambapo kwa miaka ya nyuma wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kupata matibabu.“Kupitia upasuaji huo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeokoa fedha za kitanzania zaidi ya shilingi bilioni 9.8 kutokana na huduma hii kupatikana hapa nchini”, alisema Makoba.Makoba alisema JKCI pia imezijengea uwezo nchi za jirani katika kutoa huduma na matibabu ya magonjwa ya moyo ikiwemo Hospitali ya Moyo ya Zambia, Hospitali ya King Faisal ya Rwanda, Hospitali ya Queen Elizabeth ya Malawi pamoja na hospitali mbalimbali za hapa nchini.Akizungumza kuhusu tuzo hiyo Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Asha Izina aliishukuru ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kutambua na kuthamini huduma zinazotolewa na JKCI na kusema kuwa watahakikisha wananchi wengi wanafaidika na uwepo kwa taasisi hiyo.“Tutaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuhakikisha tunawafikia watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi ili nao waweze kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na kwa wataalamu wa afya tutaendelea kuwajengea uwezo ili waweze kuwatambua na kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya moyo”, alisema Asha.
Published 2024-08-13 15:41:27 by JKCI
Zaidi ya washiriki 1000 kutoka nchi 40 wanatarajiwa kushiriki katika mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo unaoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).Mkutano huo utafanyika mwezi Aprili mwakani katika Hoteli ya Sea cliff & Spa, visiwani Zanzibar.Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kutambulisha mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kupitia mkutano huo wataalamu wa afya watafundishwa kutumia teknolojia mpya ya kutibu magonjwa ya moyo kwa kutumia njia za kisasa kama vile akili mnemba.“Mkutano wa Cardiotan 2025 utaelekeza namna ya kutibu matatizo ya magonjwa ya moyo, madaktari kutoka nchi za Afrika ni wakati wetu sasa kupitia mkutano huu kujifunza mbinu mbalimbali za kutibu wagonjwa wa moyo”, alisema Dkt. Kisenge.Kwa upande wake mwenyekiti wa maandalizi ya mkutano huo Dkt. Delilah Kimambo alisema lengo kubwa la mkutano huo ni pamoja na kukusanya wataalamu wa afya ambao wanamchango mkubwa katika sekta ya matibabu ya moyo kujadili mada zitakazohusiana na kinga, lishe na matibabu ya moyo. Dkt. Delilah alisema kupitia mkutano huo kwa mara ya kwanza JKCI inaenda kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar kuwafundisha watu ambao sio wataalamu wa afya jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa anayehitaji huduma ya kwanza na kuwaleta watu pamoja.“Kupitia mkutano wetu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo tunaenda kujadili na kuona jinsi gani tunaweza kuisaidia Afrika kwa njia rahisi kabisa ili matibabu ya moyo yaweze kupatikana kwa urahisi”, alisema Dkt. Delilah.Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Aziwa Issa Makame alisema kupitia mkutano huo utaenda kuisaidia Zanzibar kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini na wale wanaoongoza watalii wataweza kupatiwa mafunzo ambayo yataweza kuwasaidia wageni wao pale wanapopata changamoto za kiafya.Aziwa aliishukuru JKCI kwa kuwa na wazo la kupeleka mkutano huo Zanzibar na kuichagua sekta ya utalii kuwa miongoni mwa sekta zitakazopatiwa mafunzo kwani mafunzo hayo ni muhimu kuifikia jamii.“Nachukua nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa utalii kujiandikisha kwaajili ya kupatiwa mafunzo ya namna ya kumsaidia mtu anayehitaji huduma ya kwanza ili kulinda afya za watalii wetu”, alisema Aziwa.Mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wa mwaka 2025 wenye kaulimbiu “Kuimarisha huduma za moyo barani Afrika kupitia jitihada za pamoja” utakuwa mkutano wa tatu tangu kuanzishwa mkutano huo mwaka 2023 ambapo mkutano wa pili wa mwaka 2024 ulikuwa wa mafanikio makubwa ambayo uliwakutanisha wataalamu wa afya zaidi ya 500 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Published 2024-06-01 07:37:44 by JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza kwa wakazi na waumini wa KKKT Kitunda.Upimaji huo ulioanza jana unafanyika kwa siku tatu katika kambi maalumu ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services katika viwanja vya kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani jimbo la kati Usharika wa Kitunda Relini.Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Samueli Rweyemamu alisema upimaji huo umefanyika katika eneo la kanisa kuwapa nafasi watu kuonana na mchungaji kwani wapo watu wenye changamoto za familia na maisha zinazowapelekea kupata magonjwa yasiyoambukiza.“Katika kambi hii tumekuja na daktari bingwa wa saikolojioa kuangalia afya ya akili kwani tatizo la afya ya akili limekuwa kubwa katika jamii, watu wenye tatizo hilo wakirudi kwa mchungaji wakapata huduma za kiroho watakaa vizuri na kuepuka magonjwa ya shinikizo la damu”, alisema Dkt. RweyemamuDkt. Rweyemamu alisema lengo kuu la kambi hiyo ni pamoja na kufikisha huduma katika jamii, kutoa ushauri wa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kutoa huduma za matibabu endelevu kwa watu watakaogundulika kuwa na magonjwa yasiyoambukiza.“Katika kambi hii tutatoa huduma za kuchunguza na kutoa chanjo ya homa ya ini, kuchunguza na kutoa matibabu ya kansa na tezi dumu, kuchunguza na kutoa matibabu ya magonjwa ya sukari, shinikizo la damu na moyo, kuchunguza na kutoa matibabu ya matatizo ya masikio pamoja na kutoa huduma kwa watu wanaohitaji ushauri wa kimwili na kiroho”, alisema Dkt. RweyemamuKwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda aliwataka wakazi wa kitunda na maeneo ya jirani kutumia siku tatu za kambi hiyo kuwafikisha watoto kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo.Dkt. Eva alisema wazazi wakiwa na utaratibu wa kuwafanyia uchunguzi wa afya watoto wao watawasaidia kugundua matatizo ya kiafya mapema na kumpa nafasi mtoto kupata matibabu mapema kwani magonjwa mengi ya moyo kwa watoto yanakuwa na muda wa matibabu na pale muda unapovuka inakuwa ngumu kumtibu mtoto.“Kuna wakati tunakutana na changamoto za matibabu kwa watoto wenye magonjwa ya moyo kwani unakuta mtoto alihitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo kabla hajafikisha mwaka mmoja lakini kwasababu mzazi hakugundua mapema anamleta mtoto akiwa na zaidi ya mwaka mmoja hivyo kukwamisha baadhi ya matibabu”, alisema Dkt. EvaNaye Mkuu wa jimbo la kati kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani Mchungani Frank Kimambo aliwataka waumini wa KKKT kuona umuhimu wa kufanya uchungzi wa afya ili washiriki kikamilifu katika kumtumikia Mungu pamoja na kushiriki katika shughuli za kiuchumi na maendeleo kwa kuwa shughuli hizo zinahitaji watu wenye afya.Mchungaji Kimambo alisema kati ya ibada zote zilizofanyika mwaka huu katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kitunda Relini hii imekuwa ibada kubwa kwani waumini na wakazi wa kitunda wameweza kufikiwa na huduma za afya bila gharama hivyo kuushukuru uongozi wa kanisa hilo.“Nawashukuru madaktari bingwa wa JKCI, Ocean Road, Muhimbili na Hospitali ya Magereza kwa kuacha ofisi zenu na kuja kutuhudumia, Mungu amewapa uwezo kwaajili ya kushughulika na miili hii iliyoumbwa naye, nisadaka kubwa sana mmeitoa kwaajili yetu”, alisema Mchungaji KimamboUpimaji huo unafanywa na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya magereza ya Ukonga.
Published 2024-05-16 13:54:16 by JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani inafanya upimaji wa magonjwa ya shinikizo la damu, sukari na moyo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.Upimaji huo ujulikanao kwa jina la Mhe. Samia Suluhu Hassan Outreach Services umeanza kufanyika leo katika Hosptitali ya JKCI Dar Group na utamalizika kesho tarehe 17 Mei 2024 kwa kutoa huduma bila gharama kwa wananchi wote watakaojitokeza kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo.Akizungumza na waandishi wa habari daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Baraka Ndelwa alisema upimaji huo unafanyika ili kuwapa nafasi wananchi kuufahamu vizuri ugonjwa wa shinikizo la juu la damu na namna ambavyo wanaweza kujikinga na ugonjwa huo.Dkt. Baraka alisema upimaji huo unatolewa bila gharama ili kuwafikia wananchi wenye kipato cha chini kufanyiwa uchunguzi, kupatiwa matibabu na wale watakaohitaji dawa kupatiwa bila gharama.“Tunazishukuru kampuni za dawa za binadamu zilizoshirikiana nasi katika kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani kwa kuwaletea wagonjwa wetu dawa bila gharama”, alisema Dkt. BarakaKwa upande wake mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Paulina Lwegeta alisema hakujua kama ana tatizo la shinikizo la juu la damu lakini kwasababu ndugu yake ana tatizo hilo na amelazwa katika hospitali JKCI Dar Group akaamua naye atumie nafasi aliyopata kuchunguza afya yake.“Kupitia matokeo niliyoyapata hapa naona watu wengi tutakuwa tunaumwa ugonjwa wa shinikizo la juu la damu lakini hatujui, natoa wito kwa wananchi wenzangu kuwa na tabia ya kufanya vipimo mara kwa mara”, alisema PaulinaPaulina alisema amekuwa akiumwa kichwa kwa muda mrefu lakini hakujua kama ana tatizo la shinikizo la juu la damu hadi leo alipofanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa na tatizo hilo ambapo amepatiwa dawa.Omary Seif mkazi wa Temeke alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la juu la damu kwa muda mrefu na kupatiwa matibabu katika hospitali tofauti bila ya mafanikio.“Nimekuwa nikitibiwa tatizo la shinikizo la damu tangu mwaka 2022 katika hospitali tofauti lakini chaajabu hakuna siku presha yangu imeshuka na kukaa sawa, siku zote ipo juu hadi imeniletea matatizo ya macho kwani sasa hivi sioni vizuri”, alisema OmaryOmary alisema baada yakuona matangazo ya upimaji unaofanyika JKCI Dar Group alichukua hatua yakufika katika upimaji huo ambapo amepata huduma na kushauriwa vizuri kuhusu dawa alizokuwa anatumia hapo awali.Naye meneja kutoka kampuni ya dawa za binadamu ya Hetero Lab Ivan Edmund alisema kampuni mbalimbali za dawa za binadamu kwapamoja zimeungana kushirikiana na JKCI kuwapatia wananchi watakaokuta na matatizo ya shinikizo la damu, sukari na magonjwa ya moyo dawa bila gharama.Ivan alisema kulingana na hali za wananchi wengi kampuni yake na nyingine zilizojitokeza hazikuona shida kuadhimisha siku ya shinikizo la damu duniani na wananchi watakaojitokeza kupima katika kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayofanyika JKCI Dar Group.“Tunaishauri jamii iache matumizi ya dawa bila ya kumuona daktari ni vizuri kabla ya kutumia dawa ukamuona daktari akakufanyia uchunguzi na kukuandikia dawa sahihi kwani dawa ni tiba na wakati mwingine dawa inaweza kuwa sumu isipotumika vizuri”, alisema Ivan
Published 2024-05-16 10:40:26 by JKCI
Zaidi ya asilimia 60 ya watu wenye shinikizo la juu la damu hapa nchini hawajitambui kama wana tatizo hilo kwani tafiti zinaonesha kati ya watu kumi watu watatu ndio wanatambua kuwa na tatizo hilo.Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Hospitali ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group Dkt. Tulizo Shemu leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu siku ya shinikizo la damu duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Mei 17.Dkt. Shemu alisema Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu unatokana na madhara ya kiwango cha presha kuwa kikubwa katika mwili wa binadamu hivyo kusababisha shinikizo la damu kuwa juu.“Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu hauna dalili maalumu lakini zipo dalili chache zinazoweza kujitokeza endapo mtu atapata ugonjwa huu zikiwemo dalili ya kuumwa kichwa mara kwa mara, macho kutoona vizuri, moyo kwenda haraka, pamoja na kubanwa na kifua”, alisema Dkt. ShemuDkt. Shemu alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inaenda kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya upimaji bila gharama tarehe 16 na 17 May 2024 katika Hospitali ya JKCI Dar Group lengo likiwa kuleta uelewa na ufahamu katika jamii kuhusu tatizo la shinikizo la juu la damu.“Kauli mbiu ya mwaka huu inatutaka kuzifahamu tarakimu za shinikizo la damu kwa kupima presha kwa usahihi na endapo utakutwa na ugonjwa huu hakikisha unapata matibabu na kudhibiti ugonjwa ili usiweze kukuletea madhara mengine yatokanayo na tatizo la presha”, alisema Dkt. ShemuDkt. Shemu alisema kwa takwimu zilizofanyika kwa wagonjwa wanaotibiwa JKCI mwaka 2023 kati ya wagonjwa 125,927 waliopatiwa matibabu asilimia 42 walikuwa na shinikizo la juu la damu.“Madhara ya ugojwa huu ni pamoja na kupata kiharusi, kusababisha figo kushindwa kufanya kazi, kupata magonjwa ya mshtuko wa moyo, tatizo la moyo kushindwa kufanya kazi, kuvimba miguu, kupata ganzi sehemu za mwili, kupumua kwa shida, kukosa nguvu pamoja na shida za uzazi”, alisema Dkt. ShemuNaye daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sulende Kubhoja alisema tatizo la shinikizo la juu la damu huwapata pia watoto na tatizo hilo hutokana na matatizo mengine ambayo mtoto anakuwa nayo.Dkt. Kubhoja alisema tunapoenda kuadhimisha siku ya shinikizo la damu tusiwasahau watoto kuwashirikisha upande wa kufanyiwa uchunguzi na hata eneo la kupata elimu kuhusu ugonjwa huo ili pale wanapoweza kujikinga wajikinge.“Mara nyingi ukimkuta mtoto ana shinikizo la juu au la chini la damu hutokea kama mtoto ana matatizo ya figo, au matatizo mengine katika viungo vinavyowasiliana mwilini”, alisema Dkt. KubhojaDkt. Kubhoja alisema kuna watoto wamekuwa wakipata tatizo la shinikizo la juu la damu kutokana na magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa pamoja na matatizo ya mishipa ya damu kuwa na hitilafu.“Sisi tunapopata mtoto ana tatizo la shinikizo la juu la damu tunamfanyia uchunguzi kwa kuangalia kila kiungo cha mwili wa mtoto ili tuweze kutambau sehemu yenye matatizo na kuweza kuitibu” alisema Dkt. Kubhoja
Published 2024-05-06 13:18:22 by JKCI
Kwa mara ya kwanza upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo kwa watu wazima umefanyika kwa mgonjwa ambaye valvu yake ya moyo ya upande wa kushoto ilikuwa ikivujisha damu (severe mitral regurgitation).Upasuaji huo umefanywa hivi karibuni na madaktari bingwa wa upasuajia wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mwenzao kutoka Serikali ya Watu wa China.Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Williams Ramadhan alisema upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo umekuwa ukifanyika kwa watoto wenye shida za valvu lakini kwa watu wazima mgonjwa huyo amekuwa wa kwanza kurekebishiwa valvu yake kwani wagonjwa wengine wamekuwa wakiwekewa valvu za bandia.“Upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo mara nyingi umekuwa ukifanyika upande wa watoto kwa mafanikio makubwa lakini haufanywi upande wa upasuaji wa moyo kwa watu wazima kwani matibabu hayo yanahitaji utaalamu wa hali ya juu lakini pia mafanikio huongezeka pale daktari husika anapokuwa amefanya idadi kubwa ya upasuaji huo”.“Ukimfanyia mgonjwa upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo na usifanikiwe utahitaji kurudia kufanya upasuaji tena mara ya pili hivyo kumuongezea mgonjwa muda ya kukaa kwenye mashine na kumpa wasiwasi”, alisema Dkt. RamadhaniDkt. Ramadhani alisema mara nyingi kwasababu wataalamu wa JKCI wa upasuaji mkubwa wa moyo kwa watu wazima bado hawajatoa huduma hiyo kwa wagonjwa wengi wamekuwa wakifanya upasuaji wa kubadilisha valvu za moyo na si kurekebisha valvu za moyo.“Tunaushukuru uongozi wa Taasisi kutuletea mtaalamu kutoka China anayefanya upasuaji wa kurekebisha valvu za moyo kwa wagonjwa watu wazima ambao valvu zao zinaweza kurekebishwa na kupona ambaye kwa kipindi cha miaka miwili tutakachokuwa naye hapa atatuongezea ujuzi zaidi”, alisema Dkt. Ramadhan.Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Serikali ya watu wa China Liu YiMin alisema upasuaji huo kwake umekuwa wa kwanza kuufanya tangu afike katika Taasisi hiyo na kuweza kubadilishana ujuzi na wataalamu wenzake wa JKCI.Dkt. Liu alisema matibabu ya kurekebisha valvu za moyo humsaidia mgonjwa kuishi bila ya kutumia dawa za kuzui damu kuganda (Anticoagulants) katika maisha yake tofauti na mgonjwa ambaye valvu yake ya moyo imebadilishwa na kuwekewa ya bandia hulazimika kutumia dawa maisha yake yote ili kuzuia damu isigande“Mgonjwa aliyebadilishiwa valvu za moyo uhitaji kutumia dawa ya warfarin hivyo kumlazimu kupima damu yake mara kwa mara kuangalia kama inaganda tofauti na mgonjwa huyu ambaye tumemrekebishia valvu yake hivyo haitaji kutumia warfarin”, alisema Dkt. Liu YiMin.Dkt. Liu alisema wagonjwa waliobadilishiwa valvu za moyo wakati mwingine hupata tatizo la kuvuja damu hivyo kuwa katika hatari na kuhitaji kuonana na wataalamu wa afya mara kwa mara.“Upasuaji huu wa kurekebisha valvu za moyo hasa kwa wanawake huwapa wagonjwa nafasi ya kutengeneza familia kwani mwanamke anapokuwa katika kipindi cha ujauzito hatakiwi kutumia dawa mbalimbali ikiwemo dawa ya warfarin”, alisema Dkt. Liu.Naye mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kurekebisha valvu ya kushoto ya moyo kutoka mkoani Mtwara Ismail Stambuli alisema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo na shinikizo la damu kwa muda mrefu tatizo ambalo hakutegemea kama ingefikia kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo.Ismail alisema tatizo la moyo amekuwa nalo tangu utotoni na kuonyesha dalili moja ya kutokwa na jasho kwa wingi lakini kwasababu hakujua kama kutokwa na jasho kwa wingi ni dalili ya magonjwa ya moyo hakuwahi kufuatilia matibabu hadi sasa alipokuwa akisumbuliwa na typhoid mara kwa mara hivyo kulazimika kufanyiwa uchunguzi zaidi na kugundulika kuwa na tatizo la valvu ya kushoto ya moyo.“Nawashukuru sana wataalamu wa JKCI kwa kugundua tatizo langu na kulitibu kwasababu sikuwa na dalili na ilikuwa hatari kwangu maana ningeendelea na maisha kama kawaida kumbe nina tatizo kubwa katika moyo wangu”, alisema Ismail.