Published 2024-09-24 14:37:39 by JKCI
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na Hospitali ya Medanta iliyopo nchini India kubadilishana ujuzi katika fani mbalimbali za kutoa huduma za matibabu ya moyo.
Ushirikiano huo umeanza kwa mara ya kwanza jana baada ya daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Medanta kufika JKCI na kuanza kutoa huduma za upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema ujio wa daktari huyo umedhamiria kuwajengea uwezo wataalamu wa JKCI na kushirikiana kwa pamoja kubadilishana ujuzi kwa kuwafanyia upasuaji wa tundu dogo wagonjwa.
“Dkt. Chandra amefika jana na kushirikiana nasi kutoa huduma za upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa wawili na leo ataendelea nasi kuwafanyia upasuaji wa tundu dogo wagonjwa wengine watatu”, alisema Dkt. Waane
Dkt. Waane alisema Medanta ni moja ya Hospitali kubwa zinazotoa matibabu ya moyo kwa utaalamu mkubwa na sasa imeanza kushirikiana na JKCI katika kutoa huduma mbalimbali bingwa bobezi za moyo katika upasuaji wa moyo pamoja na kupokea wataalamu wa JKCI wanaopenda kuongeza ujuzi katika fani mbalimbali za matibabu ya moyo.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Medanta iliyopo nchini India Preveen Chandra alisema amekuwa akifanya upasuaji wa tundu dogo kwa utaalamu wa juu hivyo akaona ni wakati sasa kukutana na wataalamu wenzake kuona namna wanavyofanya upasuaji huo na kubadilishana ujuzi.
“Wagonjwa tunaowatibu India wanatoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo Afrika, wagonjwa hawa tumekuwa tukiwatibu kwa kutumia utaalamu mpya kila tunapopata ujuzi mpya kama vile upasuaji wa Tavi wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu bila ya kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI)”, alisema Dkt. Chandra
Dkt. Chandra alisema baada ya kufanya upasuaji na wataalamu wa JKCI ameona ni Taasisi inayokuwa kwa kasi kutokana na uwekezaji wa vifaa tiba vya kisasa vinavyotumika kutoa huduma za upasuaji wa moyo.
“Naamini baada ya miaka 10 ijayo taasisi hii itakuwa inafanya aina zote za upasuaji wa moyo zinazofanyika duniani, ushirikiano wetu na taasisi hii utaendelea kuhakikisha kila hatua inayopigwa duniani katika kutoa huduma hizi na hapa hatua hiyo inafanyika”, alisema Dkt. Chandra