Published 2024-09-03 06:13:29 by JKCI
Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma nchini wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za ushauri, upimaji na matibabu ya moyo kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Huduma hiyo ya uchunguzi iliyofanyika hivi karibuni ilitolewa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya AICC ambapo huduma zilizotolewa ni kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu, vipimo vya maabara, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi viongozi hao walisema wengi wao hawana muda wa kupima afya zao hii ni kutokana na majukumu ya kazi waliyokuwa nayo lakini kutolewa kwa huduma hiyo katika kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kumewasaidia kupata muda wa kupima afya zao.
“Kutokana na majukumu ya kazi kuwa mengi sisi viongozi huwa tunakosa muda wa kupima afya zetu na wengi wetu tunatumia dawa pale tunapojisikia vibaya, lakini katika kikao kazi hiki tumeletewa huduma hii muhimu ya kupima afya zetu, nimeona nami nije kupima afya yangu ili nijue nikoje”.
“Ninaishauri JKCI iwe na programu ya kupima afya za moyo za wafanyakazi maofisini hata kama kuna gharama za upimaji wazijulishe taasisi husika ili zigharamie, kwa kufanya hivyo wafanyakazi wengi watafikiwa na huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo”, alisema Stanley Mwonzya Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Tumbaku Tanzania.
“Tulipofika hapa tulitangaziwa kuna huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo mwenye nafasi anaweza kwenda kupima, nilifurahi kupata nafasi hii kwani kupata huduma ya upimaji wa moyo siyo jambo rahisi. Nimeonana na wataalamu na kupima vipimo vya moyo na figo namshukuru Mungu majibu yako vizuri, shida niliyonayo ni uzito mkubwa nimepewa ushauri wa kuzingatia lishe bora na kufanya mazoezi nitaenda kutekeleza ushauri niliopewa na daktari”, alishukuru Edna Mwaigomole Mwenyekiti wa Bodi ya Mamkala ya Maji Mbeya.
Allen Marwa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Kahama alishukuru kwa huduma aliyoipata ya ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo amepewa elimu nzuri ya lishe ambayo imemsaidia kujua aina gani ya vyakula ale ikiwemo mbogamboga na matunda pamoja na kufanya mazoezi.
“Ninawashauri wenzangu mahali popote pale watakapokuwa wanapopata nafasi ya kupima afya zao wapime na kama watakutwa na matatizo watapata matibabu mapema zaidi kuliko kusubiri tatizo limekuwa kubwa”, alisema Marwa.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dickson Minja alisema kwa kushirikiana na hospitali ya AICC wametoa huduma za kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa viongozi na wenye shida wamewapa rufaa ya kwenda JKCI kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.
“Mwitikio umekuwa ni mkubwa viongozi wengi wamekuja kupima afya zao na baadhi tumewapa rufaa kwaajili ya uchunguzi zaidi, ninatoa wito kwa washiriki wa mikutano mbalimbali pale kutakapokuwa na nafasi ya kupima afya wajitokeze kwa wingi na kupima afya”, alisema Dkt. Minja.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya AICC Arusha Dkt. Ezekiel Moirana alisema katika mikutano mbalimbali itakayofanyika jijini Arusha wataendelea kushirikiana na JKCI kutoa huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu ya magonjwa ya moyo kwani katika ukumbi wa AICC wanapokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi wanaohitaji huduma hiyo.
“Zoezi hili litakuwa endelevu kwani licha ya washiriki wa mkutano kupata huduma ya upimaji wa moyo ambayo tunaitoa bila malipo yoyote yale lakini pia wataalamu wetu wanajengewa uwezo na wenzao wa JKCI wa jinsi ya kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo kwani upimaji huu tunaufanya kwa pamoja”, alisema Dkt. Moirana.