Published 2024-05-06 13:10:30 by JKCI
Wananchi wametakiwa kuunga mkono jitihada za Serikali kushiriki katika mazoezi ya pamoja kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.
Rai hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akizindua mazoezi ya pamoja yaliyofanyika katika viwanja vya Coco beach jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kassim Majaliwa alisema wananchi wanatakiwa kutenga siku angalau moja kila wiki kufanya mazoezi ili kupunguza changamoto za magonjwa yasiyoambukiza.
“Mazoezi haya ya pamoja ambayo nimeyazindua rasmi leo hapa Dar es Salaam yatafanyika nchi nzima ikiwa ni mkakati wa kupunguza magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya shinikizo la damu, sukari na msongo wa mawazo”, alisema Mhe. Kassim Majaliwa
Mhe. Kassim Majaliwa alisema kuanzia leo barabara inayotoka Coco beach kuelekea daraja la tanzanite hadi makutano ya barabara ya hospitali ya Aga khan kuelekea Taasisi ya Ocean Road itakuwa ikifunga kila siku ya jumamosi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa tatu asubuhi kuwapa nafasi watu wa Dar es Salaam kufanya mazoezi bila ya kuwa na msongamano wa magari.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza hivyo kama wizara ya afya inatekeleza wajibu wake mkuu wa kuwakinga watanzania na magonjwa hayo.
“Mwaka 2016 hadi 2019 wakati nawasilisha bajeti ya wizara ya afya kati ya magonjwa kumi yanayowasumbua watanzania hakukuwa na ugonjwa hata mmoja wa magonjwa yasiyoambukiza lakini hadi kufikia mwaka 2021 magonjwa hayo yameongezeka kwa kasi hivyo kuingizwa katika bajeti ya wizara ya afya”, alisema Mhe. Ummy
Mhe. Ummy alisema mazoezi yanasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ususani magonjwa ya shinikizo la juu la damu na kisukari kwa zaidi ya asilimia hamsini.
“Wizara ya afya pamoja na kuweka nguvu kwenye kujenga hospitali na kununua dawa tutaweka nguvu kwaajili ya kuwakinga watanzania wasipate magonjwa yasiyoambukiza kwa kuhamasisha mazoezi na mtindo bora wa maisha”, alisema Mhe. Ummy
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge Kaimu Mkuu wa Hospitali ya JKCI Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alisema kufanya mazoezi kunamsaidia mtu kupunguza kiwango kikubwa cha rehemu katika mwili.
“Kila dadika kumekuwa kukitokea vifo kutokana na matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza hivyo kwakufanya mazoezi kunapunguza athari za kuweza kupoteza maisha kutokana na magonjwa hayo”, alisema Dkt. Shemu
Dkt. Shemu alisema tafiti zilizofanyika hivi karibuni zinaonyesha kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam watu wazima watano hadi sita kati ya watu 10 wana shinikizo la juu la damu ambapo wagonjwa wengi wanapata shinikizo la damu kutokana na mtindo wa maisha na kuwa na rehemu nyingi.
“Tukiwa na taratibu za kufanya mazoezi mara kwa mara tutakuwa tumeweza kupunguza kiwango kikubwa cha magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo na kuongeza nguvu kazi katika nchi yetu”, alisema Dkt. Shemu