Published 2024-05-06 13:06:10 by JKCI
Wataalamu kutoka Wizara ya Afya nchini Sierra Leone wametembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika matibabu ya moyo barani Afrika.
Wakiwa katika Taasisi hiyo wataalamu hao walijifunza namna ambavyo matibabu ya moyo yalivyoimarika nchini kutokana na mambo matatu ikiwemo utayari wa Serikali kuwekeza kwenye matatibu ya moyo.
Mbinu zingine ni Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kusambaza dawa kwenye taasisi hiyo na mfumo wa manunuzi na uendeshaji wa huduma za kifamasia unavyofanyika, ushirikiano wa watendaji ndani ya taasisi pamoja na matumizi ya mifumo ya Tehama kwenye matibabu.
Uwekezaji kwenye mifumo ya Tehama katika matibabu na utayari wa Serikali kuwekeza ni mambo aliyoyatajwa kuwa ni muhimu wakayafanyie kazi wanapokwenda kuanzisha taasisi ya moyo.
Mganga Mkuu wa Serikali ya Sierra Leone Dkt. Sarfie Kenneth ambaye aliongoza timu ya wataalamu hao 11 kuja nchini, alisema Tanzania kwenye eneo la matibabu imepiga hatua ndio maana wamekuja kujifunza.
Dkt. Keneth alisema ni muhimu kwa nchi za Afrika kushirikiana kufanya kazi kwa pamoja husasan kwenye uimarishaji wa sekta ya afya.
"Tiba nyingi za kibingwa zinafanyika nje ya mataifa ya Afrika hivyo kuwa na taasisi kama JKCI ni hatua kubwa ambapo pia tunapaswa kuweka ushirikiano, lakini tumeona utayari wa Serikali ni uti wa mgongo kwa kila kitu kufanyika", alisema Dkt. Keneth.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema matunda ya ziara hiyo ni kuvutia utalii tiba.
"Wenzetu wamekuja kujifunza namna ambavyo tumepiga hatua na tumewaeleza namna Serikali ilivyoamua kuwekeza kwenye matibabu kwa kuajiri wataalamu na kununua vifaa, pia wamejifunza kuanza kuleta wagonjwa hapa nchini kutokana na ambavyo wameona huduma zinavyotolewa na hii ni sehemu ya utalii tiba”, alisema Dkt. Kisenge.
Naye Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa JKCI Dkt. Delilah Kimambo alisema matibabu ya moyo si ya daktari peke yake bali ni ushirikiano wa wataalamu mbalimbali hivyo aliwaeleza wataalamu kutoka Sierra Leone ushirikiano wa wataalamu kwenye taasisi hiyo ndiyo kiungo muhimu kwa usalama wa wagonjwa.
Ziara hiyo ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya nchini Sierra Leone ilikuwa ni ya kujifunza namna JKCI ilivyopiga hatua na mbinu walizotumia kwa lengo la kwenda kutumia mbinu hizo kuanzisha taasisi kama hiyo nchini humo.