Wizara ya Maji yachangia matibabu ya watoto watano wenye magonjwa ya moyo
-
Author: JKCI Admin
-
Published At: Saturday, Mar 22, 2025
Wizara ya Maji pamoja na Taasisi zake imetoa mchango wa Tshs. Milioni 20 kwaajili ya kugharamia matibabu ya watoto watano wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mfano wa hundi ya mchango huo Katibu Mkuu Wizara ya Maji Eng. Mwajuma Waziri alisema suala la afya ni suala mtambuka linalopaswa kubebwa na sekta zote kuweza kurudisha tabasamu kwa watoto wanaopitia changamoto za magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo.
"Kutokana na umuhimu wa afya mwaka huu tumeamua kusherehekea wiki ya maji kwa kuwagusa watoto watano wenye magonjwa ya moyo ili kurudisha tabasamu kwao na familia zao", alisema Eng. Waziri
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dr. Angela Muhozya alisema watoto wengi wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo hufika JKCI kwa kuchelewa hivyo kuhitaji kupatiwa matibabu makubwa.
“Kama JKCI tumejikita kufanya huduma ya tiba mkoba kwa kupita katika mikoa mbalimbali kutoa huduma za upimaji na kuwajengea uwezo wataalamu waliopo mikoani ili waweze kuwagundua watoto hao mapema na kuwafikisha kwetu mapema kwaajili ya matibabu”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela alisema huduma za matibabu ya moyo ni gharama kutokana na vifaa tiba pamoja na dawa wanazohitaji kutumia, hivyo Serikali pamoja na wadau mbalimbali wamekuwa wakichangia gharama hizo kwa watoto wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu.
“Tukipata wadau wanaotushika mkono kama ambavyo nyie mmetushika tunashukuru kwani watoto wengi tunaowapa huduma hapa wanatoka mikoani hivyo ukiacha huduma za matibabu pia wanahitaji huduma nyingine ambazo wakati mwingine wanashindwa kuzimudu wanapokuwa hapa Dar es Salaam.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema takwimu za ulimwenguni zinasema katika kila vizazi hai mia moja, mtoto mmoja anazaliwa na shida ya moyo.
“Kwa upande wa Tanzania ambapo kuna takribani ya vizazi milioni mbili kila mwaka kati yao elfu ishirini wanazaliwa na magonjwa ya moyo ambapo elfu nne watahitaji matibabu mapema zaidi kabla ya umri wa mwaka moja ili kuyanusuru maisha yao”, alisema Dkt. Stella
Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ni pamoja na matundu kwenye moyo, mishipa kubana, mishipa kugeuka nk. Matatizo ya kuzaliwa nayo yanachangiwa na sababu mbalimbali yakiwemo maradhi ambayo mama anayapata wakati au kabla ya ujauzito ikiwemo kisukari, maambukizi ya maradhi ya virusi mfano rubella; matatizo haya pia yanaweza kuchangiwa na mabadiliko kwenye vinasaba vya mtoto.
Dkt. Stella alisema katika kliniki ya JKCI wanaona watoto wapya wenye shida za moyo takribani watano hadi 10 kila siku kutokea nchi nzima hivyo kusababisha orodha ya watoto wanaohitaji matibabu ya moyo kwa njia ya upasuaji mkubwa au kwa upasuaji mdogo usiohitaji kufungua kifua kuwa si chini ya mia tano, orodha inayongezeka kila kukicha.